Bomoabomoa na machafuko yawafanya watu 30,000 wabaki bila makaazi Lagos, Nigeria
Watu wapatao 30,000 wamebaki bila makaazi kufuatia zoezi la ubomoaji nyumba lililotekelezwa kwa amri ya serikali ya Nigeria pamoja na fujo na mapigano yaliyohusisha wakaazi wa jamii hasimu za maeneo ya mabanda katika jiji kuu la nchi hiyo Lagos.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Juhudi za Uadilifu na Uwezeshaji (JEI) lenye makao yake mjini Lagos limetoa taarifa na kueleza kuwa mabuldoza yaliyokuwa yakisindikizwa na askari polisi siku ya Jumatano yalibomoa na kusomba nyumba za raia katika kijiji cha Lekki na wilaya nyingine za eneo la soko.
Kwa mujibu wa asasi hiyo, maafisa wa mamlaka husika waliamua kutekeleza zoezi hilo la kubomoa nyumba licha ya amri ya mahakama ya kusimamishwa hadi shauri hilo litakaposikilizwa mahakamani.
Taasisi ya JEI imeonyesha pia filamu ya vidio inayowaonyesha watu wakikimbia kwa kutumia boti, ushahidi ambao umethibitishwa pia na mashuhuda na wakaazi wa eneo hilo.
Hata hivyo msemaji wa Polisi ya Lagos amekanusha madai kuwa polisi walibomoa nyumba za raia. Aidha amesisitiza kuwa watu kadhaa wametiwa nguvuni kwa kuchoma moto nyumba hizo.
Kisiwa cha Lekki ambacho ni kitovu cha wawekezaji kimekuwa kikivutia raia wengi masikini wa Nigeria na vibarua kutoka nchi jirani ya Benin. Eneo hilo limekuwa uwanja wa fujo na mapigano baina ya wakaazi wa nyumba za mabanda wanaowania ajira na sehemu ya kuishi.
Machafuko yalianza wiki hii baada ya kuzuka fujo na mapigano kati ya wakaazi wenyeji wa eneo hilo la mabanda na Wabenin wanaotafuta ajira.
Imeripotiwa kuwa kila siku maelfu ya wakaazi wa vijijini nchini Nigeria huelekea jiji la Lagos lenye wakaazi milioni 23.
Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa idadi ya watu nchini Nigeria itaongezeka zaidi ya mara mbili ifikapo mwaka 2050 kwa kufikia watu milioni 400 na kuwa nchi ya tatu kwa watu wengi zaidi duniani baada ya China na India.../