Sisitizo la Umoja wa Afrika la kukabiliana na kundi la Boko Haram
Viongozi wa Umoja wa Afrika wametilia mkazo udharura wa kuendelezwa uungaji mkono na misaada kwa kikosi kinachoundwa na wanajeshi wa nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika katika vita dhidi ya kundi la Boko Haram.
Balozi Smail Chergui ambaye ni Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) amezungumzia jambo hilo kwenye kikao chake na makamanda wa ngazi ya juu wa kikosi hicho kinachoundwa na wanajeshi wa nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika. Kikao hicho kiliitishwa mjini Addis Ababa katika makao makuu ya AU lengo likiwa ni kuzungumzia hali ya usalama katika eneo la magharibi mwa Afrika na athari za oparesheni ya kikosi hicho cha jeshi katika vita dhidi ya Boko Haram. Muungano huo wa kijeshi unajumuisha wanajeshi kutoka nchi za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon na umeasisiwa kwa pendekezo la Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria.
Muungano huo hadi sasa umetekeleza oparesheni kadhaa dhidi ya ngome za Boko Haram kwa minajili ya kuliangamiza kundi hilo la kigaidi. Pamoja na hayo yote bado baadhi ya maeneo huko Nigeria, kaskazini mwa Cameroon na Niger yanashikiliwa na wapiganaji wa kundi la Boko Haram.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua ya Umoja wa Afrika ya kutangaza uungaji mkono wake kwa kikosi hicho cha nchi za magharibi mwa Afrika dhidi ya Boko Haram itawatia moyo zaidi wanajeshi wa kikosi hicho. Hasa ikizingatiwa kwamba, taarifa ya umoja huo inasisitiza kwa mara nyingine tena juu ya mapambano dhidi ya Boko Haram.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ambalo lina jukumu la kusaidia juhudi za kurejesha usalama na amani katika nchi wanachama, limeunda kamati inaowajumuisha kamanda wa kikosi hicho cha jeshi cha nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika dhidi ya Boko Haram, naibu kamanda na pia mkuu wa ofisi ya AU huko Chad. Hatua hiyo imechukuliwa kwa shabaha ya kuwezesha mawasiliana zaidi baina ya makamanda wa majeshi katika eneo hilo kuhusiana na vita dhidi ya Boko Haram.
Viongozi wa nchi za Kiafrika hivi karibuni walitilia mkazo suala la kuangamizwa kikamilifu makundi ya kigaidi kama Boko Haram huko Nigeria na al Shabab huko Somalia. Viongozi hao wanatambua vyema mfungamano na uhusiano wa karibu uliopo kati ya usalama wa kudumu na ustawi wa kiuchumi na kisiasa na ni kwa sababu hiyo ndio maana wakaliweka lengo hilo katika ajenda yao yao kuu.
Bara la Afrika limeathiriwa na matukio ya Libya; suala ambalo limezidisha hofu na wasiwasi kutokana na kuendelea mapigano nchini humo. Vilevile wasiwasi kuhusu taathira mbaya za baadaye za mapigano na vita vya Libya, ulikwua sababu ya mkutano wa viongozi wa nchi jirani za Libya wiki iliyopita katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa kuzungumzia matukio ya Libya.
Hatari ya kuenea ugaidi ni suala linalozihusu nchi zote za Kiafrika na tunaweza kusema kuwa, hatari hiyo inaweza kupanuka zaidi na kuvuka mipaka ya bara hilo. Ndio maana Umoja wa Afrika umetaka kuangamizwa na kutokomezwa kikamilifu makundi ya al Shabab na Boko Haram. Hata hivyo kufanikiwa lengo hilo kunahitajia ushirikiano wa kisiasa na kiusalama kama ule uliopelekea kuanzishwa muungano wa majeshi ya magharibi mwa Afrika.