Jeshi la Somalia lakomboa eneo jengine kutoka kwa ash Shabab
Jeshi la Somalia limefanikiwa kukomboa eneo jengine katikati mwa nchi hiyo kutoka mikononi mwa kundi la wakufurishaji la ash Shabab.
Abdullahi Muhammad, mmoja wa makamanda wa jeshi la Somalia amenukuliwa na vyombo vya habari akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, jeshi la nchi hiyo kwa kusaidiwa na kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM jana kilifanikiwa kukomboa aneo jingine muhimu katikati ya Somalia kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la ash Shabab.
Kwa mujibu wa duru za Somalia, kundi hilo limeshafurushwa kutoka katika miji yote muhimu ya nchi hiyo na hivi sasa limekimbilia katika maeneo ya vijijini huko katikati na kusini mwa Somalia. Pamoja na hayo limekuwa likifanya mashambulizi ya hapa na pale hata katika mji mkuu Mogadishu.
Aidha kundi la ash Shabab limesema litaharibu uchaguzi wa Somalia, suala ambalo limelifanya jeshi na kikosi cha AMISOM kuweka ulinzi mkali katika maeneo na vituo vya kupigia kura.
Hivi sasa Somalia inajiandaa kufanya uchaguzi wa Rais tarehe 31 mwezi huu wa Novemba. Uchaguzi wa bunge unaendelea kufanyika hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.