ICC yataka maelezo kuhusu mauaji ya Waislamu wa Shia nchini Nigeria
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imeitaka serikali ya Nigeria kutoa maelezo kuhusu mauaji yaliyofanywa mwaka jana na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Zaria.
Kituo cha habari cha All Africa kimeripoti kuwa, baada ya wito huo wa ICC, Waziri wa Sheria wa Nigeria ambaye pia ni Mwendesha Mashtaka Mkuu wa nchi hiyo, Abubakar Malami ameelekea The Hagua nchini Uholanzi kwa ajili ya kueleza nafasi ya jeshi la nchi yake katika mauaji hayo.
Wakati huo huo wajumbe wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walifanya maandamano jana katika mji wa Abuja wakipinga mauaji yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wasiopungua mia moja katika mji wa Kano siku ya Jumanne iliyopita. Waandamanaji hao walisema kuwa, Jeshi la Polisi ya Nigeria liliwashambulia na kuwaua kwa kuwapiga risasi Waislamu zaidi ya mia moja waliokuwa katika shughuli ya kidini itakayofika kileleni Jumapili ijayo ambayo ni maarufu kwa jina la Arubaini ya Imam Hussein tangu baada ya tarehe 10 mwezi Muharram wakati mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) alipouliwa shahidi.
Waandamanaji hao wamelitaka Baraza la Haki za Binadamu la Taifa kuwasilisha ujumbe wao kwa Rais Muhammadu Buhari na kutangaza kuwa, Waislamu nchini Nigeria ni raia kama walivyo raia wengine na wana haki ya kulindwa mbele ya ukatili unaovuruga amani na kuangamiza wanadamu.
Wimbi la mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria lilianza tarehe 13 Disemba mwaka jana baada ya jeshi la nchi hiyo kushambulia kituo cha kidini cha Baqiyyatullah katika mji wa Zaria na kuua mamia ya Waislamu wakiwemo watoto watatu wa kiongozi ya Harakai ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky.