Serikali ya Nigeria yabomoa majengo ya harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19792-serikali_ya_nigeria_yabomoa_majengo_ya_harakati_ya_kiislamu_ya_nchi_hiyo
Serikali ya Nigeria imeendeleza ukandamizaji dhidi ya Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo kwa kubomoa majengo kadhaa ya harakati hiyo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Nov 19, 2016 12:14 UTC
  • Serikali ya Nigeria yabomoa majengo ya harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo

Serikali ya Nigeria imeendeleza ukandamizaji dhidi ya Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo kwa kubomoa majengo kadhaa ya harakati hiyo.

Viongozi wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamesema vyombo vya dola vimebomoa majengo kadhaa ya harakati hiyo ikiwemo skuli, hospitali na vituo vya masomo ya dini katika miji ya Zaria na Saminaka katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo.

Viongozi hao wa harakati ya Kiislamu Nigeria aidha wamebainisha kuwa ubomoaji huo umefanyika bila ya kutolewa taarifa kabla na ilhali harakati hiyo haikuwa imefanya kitendo chochote cha kuichochea serikali kuchukua hatua ya kijinai ya kusababisha maafa kama hayo.

Waislamu wa Nigeria wakishiriki katika matembezi ya Arubaini 

Ubomoaji huo umefanywa baada ya vikosi vya usalama vya Nigeria kuwaua wanachama wapatao 100 wa harakati ya Kiislamu waliokuwa wakishiriki kwenye maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein (AS).

Katika tukio hilo lililotokea siku ya Jumatatu, askari usalama wa Nigeria waliwashambulia Waislamu wa Kishia waliokuwa katika maombolezo hayo kwa kutumia risasi moto na mabomu ya kutoa machozi. 

Tangu mwaka uliopita hadi sasa harakati ya Kiislamu Nigeria na wafuasi wake wamekuwa wakikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa serikali ya nchi hiyo.

Sheikh Ibrahim Zakzaky alivyoshambuliwa na kujeruhiwa na jeshi la Nigeria

Wimbi la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria lilianza tarehe 13 Desemba mwaka jana, wakati jeshi lilipowaua na kuwajeruhi Waislamu wengi katika shambulio dhidi ya kituo cha kidini cha Husainiyyah ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria. Katika shambulio hilo, jeshi hilo lilimjeruhi vibaya, kisha likamkamata na kumweka korokoroni pia kiongozi wa harakati ya Kiislamu Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe.../