Kuongezeka ukandamizaji wa Waislamu nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19873-kuongezeka_ukandamizaji_wa_waislamu_nchini_nigeria
Wanajeshi wa serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria wameendelea kuwakandamiza Waislamu wa nchi hiyo kwa kuvunja nyumba na maeneo yanayomilikiwa na Waislamu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2016 23:33 UTC
  • Kuongezeka ukandamizaji wa Waislamu nchini Nigeria

Wanajeshi wa serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria wameendelea kuwakandamiza Waislamu wa nchi hiyo kwa kuvunja nyumba na maeneo yanayomilikiwa na Waislamu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Wakuu wa harakati hiyo ya Kiislamu wamesema kuwa, serikali ya Rais Buhari imechukua hatua hizo za ukandamizaji dhidi ya harakati hiyo bila ya kutoa onyo lolote kabla yake na wala harakati hiyo haikufanya jambo lolote lile la kuichokoza serikali au kuvunja sheria.

Uharibifu huo wa maeneo ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria umekuja baada ya ukatili wa siku ya Jumamosi uliofanywa na wanajeshi wa serikali wa kuwashambulia kinyama na kuua shahidi zaidi ya Waislamu 100 waliokuwa kwenye kumbukumbu za Arubaini ya Imam Husain AS.

Rais Muhammadu Buhari (kushoto) akiwa na mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz

 

Kwenye ukandamizaji huo, wanajeshi wa serikali walitumia risasi za kivita na gesi za kutoa machozi kuwakandamiza Waislamu waliokuwa kwenye maombolezo, kaskazini mwa nchi hiyo.

Wimbi la ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Nigeria lilianza tarehe 12 Disemba mwaka jana wakati wanajeshi wa serikali walipovamia Husainia moja katika mji wa Zaria wa jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria.

Katika uvamizi huo, Sheikh Ibrahim Zakzaki, mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alijeruhiwa vibaya, mamia ya Waislamu wakauawa shahidi wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaki. Hivi sasa karibu mwaka mmoja umepita, Sheikh Zakzaki yuko kizuizini akiishi katika mazingira magumu huku wanajeshi wa Nigeria wakiendelea na wimbi la mashambulizi yao dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo, bila ya huruma.

Zaidi ya nusu ya wananchi wa Nigeria ni Waislamu. Muda wote Waislamu wa nchi hiyo walikuwa wakiishi kwa usalama na amani na watu wa dini nyinginezo. Hata hivyo uchochezi wa madola ya kigeni pamoja na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kujinufaisha binafsi umezusha mifarakano nchini humo na kuwakosesha Waislamu utulivu na wakati huo huo kupata kisingizio cha kufanya ukandamizaji mkubwa dhidi yao hususan katika maeneo yenye Waislamu wengi ya kaskazini mwa Nigeria. 

Wanajeshi wa Nigeria wakifanya mauaji dhidi ya Waislamu wa Zaria.

 

Hivi karibuni viongozi wa jimbo la Kaduna walipiga marufuku shughuli zote za Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Viongozi hao walidai kuwa miongoni mwa adhabu zitakazotolewa na mtu yeyote anayejishughulisha na harakati hiyo ni kifungo cha maisha jela na faini kubwa ya fedha taslimu. Si hayo tu lakini pia viongozi hao wa jimbo la Kaduna walipiga marufuku mikusanyiko yoyote ya Waislamu.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuongezeka mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria na kuendelea kuwekwa kizuizini Sheikh Zakzaki kinyume cha sheria kunafanyika kwa lengo la kuzuia kukua na kuongezeka harakati za Kiislamu na kupunguza nafasi ya Waislamu nchini humo.

Kwa miaka mingi sasa Mawahabi wakiongozwa na Saudi Arabia wamekuwa wakiwashinikiza viongozi wa nchi hiyo wachukue hatua za ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo.

Nigeria inahitaji umoja na mshikamano kupambana na magenge ya waasi kaskazini na kusini mwa nchi hiyo na sio kukandamiza Waislamu wanaoshi kwa salama na wananchi wengine

 

Serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria imeamua kuelekeza nguvu zake katika kukandamiza Waislamu ambao walikuwa wanaishi kwa salama na amani na wananchi wengine katika hali ambayo nchi hiyo inakabiliwa na matatizo mengi kama vile mashambulizi ya genge la Boko Haram, hali mbaya ya kiuchumi na ukosefu wa usalama na amani unaosababishwa na magenge ya waasi kusini mwa nchi hiyo. Weledi wa mambo wanasema kuwa, serikali ya Nigeria inapaswa kutambua kuwa nchi hiyo inahitajia mno umoja na mshikamano wa watu wake hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote, ili iweze kujikwamua kutoka kwenye matatizo hayo yanayoikabili. Ni jambo lililo wazi kuwa, kuendelea kuwakandamiza Waislamu si njia ya kuleta umoja na mshikamano nchini humo.