Malalamiko dhidi ya kuharibiwa majengo ya Harakati ya Kiislamu Nigeria
Mwanachama wa ngazi za juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amelaani vikali hatua ya serikali ya jimbo la Kaduna lililoko katikati mwa nchi hiyo, ya kuharibu na kubomoa majengo ya harakati hiyo.
Akizungumza hapo jana Jumapili, Abdulmumuni Giwa, mwanachama wa ngazi za juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amelaani kitendo hicho cha uhalifu cha serikali ya Kaduna akisisitiza kuwa kinakiuka wazi haki ya kisheria ya raia wa nchi hiyo ya kuabudu na kutekeleza majukuu yao ya kidini kwa uhuru kamili. Amesema, kitendo hicho cha serikali ya Kaduna vilevile kinakiuka wazi katiba ya nchi hiyo ambayo inampa kila Mnigeria haki ya kuabudu na kutekeleza ibada zake kwa uhuru kamili.
Hivi karibuni serikali ya jimbo hilo la Kaduna iliamuru askari usalama wa jimbo hilo kuharibu majengo kadhaa yanayomilikiwa na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, zikiwemo shule, hospitali na hauza za harakati hiyo katika mji wa Zaria ulioko kwenye jimbo hilo. Kitendo hicho kimetekelezwa wiki moja baada ya polisi katika jimbo la Kano kuwafyatulia risasi wanachama wa Harakati ya Kiislamu wakiokuwa wakitembea kwa amani katika makumbusho ya Siku ya Arubaini ya kuuawa Imam Hussein (as) ambapo waandamanaji 100 kati yao waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa vibaya kutokana na ufyatuaji huo wa risasi pamoja na vitoa machozi.