Waislamu wa Kishia Nigeria walaani kubomolewa shule zao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20059-waislamu_wa_kishia_nigeria_walaani_kubomolewa_shule_zao
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imelaani kitendo kilicho kinyume na sheria cha viongozi wa jimbo la Kaduna nchini humo cha kubomoa shule zao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 23, 2016 23:31 UTC
  • Waislamu wa Kishia Nigeria walaani kubomolewa shule zao

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imelaani kitendo kilicho kinyume na sheria cha viongozi wa jimbo la Kaduna nchini humo cha kubomoa shule zao.

Ibrahim Musa, Mkuu wa Ofisi ya Habari ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema baada ya kubomolewa shule za harakati hiyo katika mji wa Zaria kwenye jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria kuwa, askari usalama na wafanyakazi wa serikali katika jimbo la Kaduna wameharibu na kubomoa shule za Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria pamoja na Husainiya ambayo ilikuwa haijamalizika kujengwa mjini Saminica.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema kuwa bomoa bomoa hiyo ambayo imefanywa wiki moja iliyopita ni kinyume cha sheria; na kwamba hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kabla ya kubomolewa shule hizo na wala hakukuwa na amri yoyote ya mahakama iliyoagiza kuchukuliwa hatua hiyo. Serikali ya Nigeria imeshadidisha ukandamizaji na utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini humo katika mwaka mmoja uliopita. Itakumbukwa kuwa, wanajeshi wa Nigeria mwaka jana walikivamia kituo cha Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo na kuwauwa mamia ya watu na pia kumjeruhi kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky na kumpeleka mahali kusikojulikana.

Sheikh Ibrahim Zakzaky

Hivi sasa umepita takribani mwaka mmoja tangu Sheikh Ibrahim Zakzaky alipotiwa mbaroni na kushikiliwa korokoroni huku makundi ya kiraia nchini Nigeria yakipaza sauti kwa pamoja na Waislamu yakitaka kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.