Kikao cha kusikiliza kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky chaakhirishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20272-kikao_cha_kusikiliza_kesi_ya_sheikh_ibrahim_zakzaky_chaakhirishwa
Kikao cha kusikiliza kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kimeakhirishwa na kupangiwa tarehe nyingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 27, 2016 03:51 UTC
  • Kikao cha kusikiliza kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky chaakhirishwa

Kikao cha kusikiliza kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kimeakhirishwa na kupangiwa tarehe nyingine.

Afisa mmoja wa mahakama ya Abuja ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa, kesi hiyo imeakhirishwa kutokana na kutokuja mahakamani hakimu wa faili la kesi hiyo. 

Taarifa zaidi zinasema kuwa, sasa kesi hiyo itasikilizwa tena tarehe Pili ya mwezi ujao wa Disemba. Kesi ilikuwa isikilizwe kutokana na wakili wa Sheikh Ibrahim Zakzaky kuwasilisha malalamiko ya kuendelea kushikiliwa mteja wake bila ya kufunguliwa mashtaka.

Sheikh Ibrahim Zakzaky amekuwa akishikiliwa na vyombo vya usalama vya Nigeria kwa karibu mwaka mmoja sasa bila ya kufunguliwa mashtaka hatua ambayo imekuwa ikilalamikiwa na taasisi za kutetea haki za binadamu.

Waislamu wa Nigeria wakiandamana kutaka kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky

Tangu mwanazuoni huyo atiwe mbaroni, takwa kuu la jamii ya Waislamu nchini Nigeria ni kuachiliwa huru mwanaharakati huyo wa Kiislamu na kuheshimiwa haki zake za kibinadamu. Aidha jamii ya Waislamu nchini Nigeria inaitaka serikali ya nchi hiyo iheshimu haki za Waislamu wa nchi hiyo. 

Disemba 13 mwaka jana jeshi la Nigeria lilifanya hujuma dhidi ya Husseiniyah ya Baqiyatullah na makazi ya Sheikh Zakzaky mjini Zaria. Waislamu wapatao elfu mbili waliuawa kwa umati na jeshi hilo likamtia mbaroni Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky imezorota huku maafisa wa usalama wakizuia mwanazuoni huyo kupatiwa matibabu.