Rwanda kuchunguza kuhusika Wafaransa katika mauaji ya kimbari
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Rwanda imeanzisha uchunguzi wa jinai kuhusu kuhusika raia 20 wa Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi
Ingawa majina hayo hayajatangazwa lakini ripoti ya hivi karibuni ya Tume ya Kitaifa ya Kupambama na Mauaji ya Kimbari imesema maafaisa wa ngazi za juu katika Idara za Kidiplomasia na Kijeshi Ufaransa walihusika katika kutayarisha na kutekeleza mauaji ya kimbari Rwanda yaliyopelekea watu karibu milioni moja kupoteza maisha.
Taarifa iliyotiwa saini na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Rwanda Richard Muhumuza imesema maafisa wengine zaidi wa Ufaransa, mbali na hao 20, huenda wakatakiwa watoe ushahidi. Amesema tayari wameshawasiliana na wakuu wa Ufaransa kuhusu kesi hizo.
Ripoti za huko nyuma zinaonyesha kuwa, mabalozi wa Ufaransa waliohudumu Rwanda kati ya mwaka 1990-1994 na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa Ufaransa wakati huo walihusika katika mauaji ya kimbari yaliyojiri kati ya Aprili 7 hadi Julai 3 mwaka 1994.
Katika kilele cha mauaji ya kimbari Rwanda, Ufaransa ilitumia ushawishi wake kupata idhini ya Umoja wa Mataifa kutuma kikosi cha kijeshi ilichodai kuwa ni cha kibinaadamu. Kikosi hicho badala ya kuzuia mauaji kilichochea ukatili dhidi ya Watutsi hasa katika maeneo ya magharibi na kusini mwa Rwanda.
Serikali ya Ufaransa ilikuwa muitifaki mkubwa wa serikali ya Rwanda iliyotekeleza mauaji ya kimbari kabla ya kuangushwa na harakati ya RPF iliyoongozwa na rais wa sasa Paul Kagame.