MDC: Tsvangirai atawania urais 2018 licha ya hali yake ya afya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20590-mdc_tsvangirai_atawania_urais_2018_licha_ya_hali_yake_ya_afya
Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe MDC kimesema kiko imara licha ya kuugua kiongozi wake Morgan Tsvangirai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2016 03:42 UTC
  • MDC: Tsvangirai atawania urais 2018 licha ya hali yake ya afya

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe MDC kimesema kiko imara licha ya kuugua kiongozi wake Morgan Tsvangirai.

Katibu Mkuu wa chama cha MDC cha nchini Zimbabwe Douglas Mwonzora amenukuliwa na shirika la habari la News 24 la Afrika Kusini akisema kuwa, hali ya kiafya ya Tsvangirai ambaye anaugua saratani ya utumbo mpana inazidi kuimarika kutokanana matibabu anayoyapata huko Afrika Kusini, tangu mwezi Juni mwaka huu na kusisitiza kuwa, ugonjwa wake hauwezi kumzuia kufanya kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka 2018.

Morgan Tsvangirai, mkuu wa upinzani Zimbabwe

Baada ya kutoweka katika ulingo wa siasa na vyombo vya habari kwa kipindi kirefu, Jumamosi iliyopita Tsvangirai aliwahutubia maelfu wa wafuasi wake mjini Harare, na kuwahakikishia kuwa yuko imara na wala hakuna haja ya kuundwa muungano mkuu wa upinzani kama ilivyopendekezwa na wanasiasa wa upinzani. Alisema kinachostahili kufanywa sasa ni kushinikiza marekebisho katika mfumo wa kupiga kura ili uchaguzi wa 2018 uwe huru na wa haki na ambao utaakisi matakwa ya wananchi.

Kabla ya hapo, mara ya mwisho Tsvangirai kuonekana katika uga wa siasa ilikuwa Aprili mwaka huu, wakati ambapo maelfu ya wananchi wa taifa hilo walishiriki katika maandamano dhidi ya serikali. Akizungumza mbele ya wafuasi wake Tsvangirai amesisitiza kuwa, Mugabe ameshindwa kutatua migogoro ya nchi hiyo na kwamba wananchi wa Zimbabwe wanaamini kuwa, serikali yake haina njia nyingine ila kuporomoka tu.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Robert Mugabe ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 92, amekuwa rais wa Zimbabwe tangu nchi hiyo ijipatie uhuru mwaka 1980, na hivi karibuni aliwaahidi wafuasi wake kuwa atagombea tena uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwaka 2018.