Kuendelea kuhukumiwa wafanya mauaji ya kimbari nchini Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20749-kuendelea_kuhukumiwa_wafanya_mauaji_ya_kimbari_nchini_rwanda
Licha ya kupita miaka zaidi ya 20 tangu yalipotokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda, watendaji ya jinai hizo wanaendelea kuhukumiwa hadi leo hii.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 05, 2016 00:26 UTC
  • Kuendelea kuhukumiwa wafanya mauaji ya kimbari nchini Rwanda

Licha ya kupita miaka zaidi ya 20 tangu yalipotokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda, watendaji ya jinai hizo wanaendelea kuhukumiwa hadi leo hii.

Mahakama moja nchini Ufaransa imepasisha kifungo cha miaka 25 jela dhidi ya mkuu wa zamani wa usalama wa taifa wa Rwanda baada ya kumpata na hatia ya kufanya mauaji ya kimbari mwaka 1994 nchini humo.

Pascal Simbikangwa (56) ambaye alikuwa askari wa kikosi cha ulinzi wa Rais wa zamani wa Rwanda amepatikana na hatia pia ya kufanya jinai dhidi ya binadamu kabla ya kukata rufaa mwezi Oktoba. Hivi sasa mahakama ya Ufaransa imetupilia mbali rufaa yake na kupasisha hukumu ya kufungwa jela miaka 25.

Wakati huo huo, duru za mahakama za Rwanda zimetangaza kuwa, zimeanzisha uchunguzi kuhusiana na nafasi ya maafisa 20 wa Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ya nchini humo.

 

Richard Muhumuza, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Rwanda amesema kwamba, kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa hadi hivi sasa, maafisa hao 20 wa Ufaransa wanafuatiliwa na vyombo vya mahakama ili kubaini ni kiwango gani walihusika kwenye mauaji hayo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maafisa wengine wa Ufaransa huenda nao wakatakiwa kufika mbele ya mahakama za Rwanda kujibu tuhuma za kuhusika na jinai hiyo.

Wimbi la mauaji ya kimbari liliikumba Rwanda mwaka 1994 baada ya kutunguliwa ndege ya Juvenal Habyarimana, rais wa wakati huo wa Rwanda karibu na Kigali. Habyarimana alikuwa anarejea nchini humo akitokea Arusha Tanzania alikofikia makubaliano na wapinzani.

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yanahesabiwa kuwa ni maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Karibu watu milioni moja hasa wanawake na watoto wadogo waliuliwa kinyama na Wahutu wenye misimamo mikali. Wanawake na watoto karibu 200 hadi 500 walinajisiwa kwenye jinai hiyo ya kutisha. 

Pascal Simbikangwa, akiwa mahakamani nchini Ufaransa

 

Jinai zote hizo zilifanyika mbele ya kimya cha taasisi za kimataifa, hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo halikuidhinisha mashirika ya kimataifa kuingilia mgogoro huo kwa madai kuwa ulikuwa ni mgogoro wa ndani ya Rwanda. Baya zaidi ni kuwa Umoja wa Mataifa ulikwepa hata kutumia neno mauaji ya kimbari kuhusu jinai hizo. Jamii ya kimataifa iliachia mauaji ya kinyama na kikatili yafanyike kwa miezi kadhaa nchini Rwanda ndipo ikachukua msimamo baada ya kushinikizwa vikali na fikra za walio wengi.

Hata Kofi Anna, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa alisema mara baada ya kuchukua cheo hicho kuwa hatupaswi kusahau hata mara moja kwamba jamii ya kimataifa ilishindwa kuzuia mauaji ya watu laki nane, wanawake na watoto wadogo wasio na hatia. Hatupaswi kusahau kwamba tulishindwa kutekeleza wajibu wetu wa kuzuia mauaji hayo.

Kwa miaka mingi sasa serikali ya Rwanda inajaribu kuwarejesha nyumbani waliofanya mauji hayo kwa ajili ya kuhukumiwa. Kwa mujibu wa serikali ya Kigali, sehemu kubwa ya walioshiriki kwenye mauaji hayo ya umati wanaishi katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda. Jambo hilo limesababisha kuingia matatizoni uhusiano wa Rwanda na baadhi ya nchi hizo.

 

Nchi ya Ulaya ya Ufaransa ni miongoni mwa watuhumiwa nambari moja wa jinai dhidi ya binadamu zilizotokea nchini Rwanda mwaka 1994. wakati wa mauaji hayo, Ufaransa ilikuwa rafiki wa karibu sana wa serikali ya Wahutu na kulikuwa na idadi kubwa ya wanajeshi na raia wa Ufaransa nchini Rwanda. Kwa miaka mingi sasa uhusiano wa Ufaransa na Rwanda umeshindwa kurejea katika hali iliyokuwepo kabla kutokea mauaji hayo ya mwaka 1994. Nchi nyingine ambazo mahakama zake zinafuatilia kesi za waliofanya mauaji hayo ni Canada na Uholanzi.

Amma jambo moja liko wazi nalo ni kuwa, matatizo mengi yanayotokea katika nchi mbalimbali za dunia hususan za Afrika, yana uhusiano na ukoloni na dhulma zilizofanywa na Wazungu wa Ulaya barani Afrika. Matatizo kama mizozo, mifarakano, vita vya kikabila, kikaumu na kidini ni katika urithi mchungu uliobakishwa nyuma na madola ya kikoloni ya Ulaya. Taasisi za kimataifa nazo zimedhihirisha wazi udhaifu wao wa kushindwa kukabiliana na majanga ya kibeberu yanayoshuhudiwa leo hii katika kona mbalimbali za dunia.