Dec 06, 2016 15:46 UTC
  • Kamanda wa LRA ya Uganda kizimbani ICC; akanusha mashitaka

Kamanda wa zamani wa kundi la waasi wa kaskazini mwa Uganda wa Lord's Resistance Army (LRA) amekanusha mashtaka dhidi yake mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Dominic Ongwen, ameiambia mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi kuwa, binafsi alitekwa nyara akiwa kijana barobaro na kulazimishwa kujiunga na harakati za wapiganaji wa msituni wa LRA mwishoni mwa miaka ya 80, huku akikanusha mashtaka 70 yanayomkabili, yakiwemo ya mauaji na ubakaji.

Dominic Ongwen mbele ya ICC

Ongwen ambaye kesi yake imeanza kusikilizwa leo, miezi tisa baada ya ICC kuthibitisha kuwa ana mashitaka ya kujibu, amekanusha mashtaka yote dhidi yake na kusisitiza kuwa, waasi wa LRA ndio waliotekeleza jinai hizo dhidi ya binadamu kaskazini mwa Uganda na kwamba yeye binafsi haungi mkono harakati za kundi hilo.

Majaji wa ICC awali walikataa ombi la mawakili wa Ongwen, waliotaka mteja wao afanyiwe uchunguzi wa kiakili kabla ya kuanza kusikilizwa kesi hiyo.

Kundi la waasi la LRA lilianzisha harakati zake nchini Uganda na baadaye likapanua wigo wa harakati hizo hadi katika nchi za Sudan Kusini, Chad na hata katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ongwen akiwa misituni pamoja na wapiganaji wenzake wa LRA

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kundi la waasi wa Uganda la Lord's Resistance Army (LRA) limeua zaidi ya watu laki moja na kuteka nyara watoto elfu sitini ambao baadhi yao wanatumiwa kama watumwa wa ngono.

Tags