Rais wa Ghana: Upinzani unawashawishi wafuasi wake wasikubali matokeo ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20917-rais_wa_ghana_upinzani_unawashawishi_wafuasi_wake_wasikubali_matokeo_ya_uchaguzi
Rais John Dramani Mahama wa Ghana amemtuhumu kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo kuwa anawashawishi wafuasi wa chama chake wasikubali matokeo ya uchaguzi wa Rais na Bunge unaofanyika leo nchini humo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Dec 07, 2016 00:28 UTC
  • Rais wa Ghana: Upinzani unawashawishi wafuasi wake wasikubali matokeo ya uchaguzi

Rais John Dramani Mahama wa Ghana amemtuhumu kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo kuwa anawashawishi wafuasi wa chama chake wasikubali matokeo ya uchaguzi wa Rais na Bunge unaofanyika leo nchini humo.

Mahama ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, upinzani nchini humo umewaandaa kisaikolojia wafuasi wao kutokubali matokeo ya uchaguzi huo iwapo watashindwa.

Amesema, na hapa tunamnukuu: "Hakuna hata siku moja kiongozi wa upinzani amepanda jukwaani na kuwataka wafuasi wake wadumishe amani na kuepuka ghasia, vyovyote vile yatakavyokuwa matokeo ya uchaguzi huu."

Rais John Dramani Mahama wa Ghana

Hata hivyo msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha NPP, Nana Akomea amekadhibisha madai hayo na kusisitiza kuwa chama hicho daima kimekuwa kikitoa wito wa kufanyika uchaguzi wa amani na kwamba, yote hayo yatategemea iwapo uchaguzi wenyewe utakuwa huru na wa haki.

Siku ya Jumatatu wanaharakati wa kisiasa na vyama vinavoshiriki kwenye uchaguzi wa Rais na Bunge nchini Ghana walisaini hati ya mapatano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Accra na kutilia mkazo udharura wa kuzuia kutokea aina yoyote ya machafuko kutoka kwa wafuasi wa wagombea wa makundi mbalimbali wanaoshiriki katika uchaguzi huo; sambamba na kutaka kudhaminiwa kikamilifu ulinzi na usalama na kuzingatiwa madai ya kisheria ya wanaharakati wote wa kisiasa.

Rais Mahama na kiongozi wa upinzani, Nana Akufo-Addo

Mahama ambaye alishika hatamu za uongozi mwaka 2013 baada ya kuaga dunia rais wa wakati huo, John Atta Mills, atachuana na kiongozi wa upinzani Nana Akufo-Addo katika uchaguzi wa Rais na Bunge uliopangwa kufanyika leo.

Ghana ni moja ya nchi chache za Afrika zenye kuheshimu misingi ya demokrasia na zenye historia ya kushuhudia mchakato wa amani wa kukabidhi madaraka kutoka serikali moja hadi nyingine.