UN: Boko Haram ingali tishio licha ya kupoteza ngome zake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20998-un_boko_haram_ingali_tishio_licha_ya_kupoteza_ngome_zake
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lenye makao yake nchini Nigeria lingali tishio katika eneo la Ziwa Chad licha ya kupoteza udhibiti wa ngome zake nyingi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 08, 2016 07:32 UTC
  • UN: Boko Haram ingali tishio licha ya kupoteza ngome zake

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lenye makao yake nchini Nigeria lingali tishio katika eneo la Ziwa Chad licha ya kupoteza udhibiti wa ngome zake nyingi.

Francois Lounceny Fall, Mjumbe wa UN katika eneo la Afrika ya Kati, hapo jana aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, licha ya kuwa magaidi hao wamekimbia eneo la Ziwa Chad baada ya kufurushwa na vikosi vya kieneo, lakini kundi hilo la kigaidi linasalia kuwa tishio kwa usalama wa eneo hilo.

Ameongeza kuwa, mbali na operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi hao, kuna haja ya kutafuta kiini cha watu wa matabaka mbali mbali kujiunga na makundi hayo yenye misimamo ya kuchupa mipaka, ikiwemo kadhia ya umasikini.

Wanamgambo wa Boko Haram

Duru za habari zinaarifu kuwa, kufikia sasa wakimbizi wa Nigeria wapatao laki 2.4 wamekimbilia nchi za Cameroon, Chad na Niger, kutokana na kushadidi mashambulio ya Boko Haram katika majimbo ya Adamawa, Yobe na Borno.

Hii ni katika hali ambayo, Geoffrey Onyeama, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nigeria amenukuliwa mara kadhaa akisisitiza juu ya ulazima wa kushadidishwa operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa mashambulio ya Boko Haram nchini Nigeria hadi sasa yamesababisha zaidi ya watu elfu ishirini kuuawa na wengine milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.