Snowden: Marekani na Uingereza zilimfanyia ujasusi Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya
-
Rais Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya
Nyaraka zilizotolewa na afisa wa zamani wa Wakala wa Usalama wa Taifa wa Marekani zimefichua kuwa mashirika ya kijasusi ya nchi hiyo na yale ya Uingereza yalizifanyia ujasusi nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na Rais wa Kenya.
Gazeti la Le Monde la nchini Ufaransa limemnukuu Edward Snowden, afisa wa zamani wa shirika la NSA la usalama wa taifa la Marekani akisema kuwa, viongozi, watu muhimu wa kisiasa na kiuchumi, harakati za waasi, mashirika ya mawasiliano pamoja na mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi barani Afrika yanafanyiwa ujasusi na Marekani na Uingereza ikiwa ni pamoja na kudukuliwa kwa siri mazungumzo yao.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la nchini Ufaransa, karibu nchi 20 za Afrika zilikuwa zinamulikwa kiupelelezi na satalaiti za kijasusi na vyombo vya siri vya Marekani na Uingereza katika kipindi cha miaka ya 2008 hadi 2011.
Gazeti hilo limeandika, mazungumzo ya Rais Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya na washauri wake wakuu pamoja na Raila Odinga wakati alipokuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo yalidukuliwa na kusikilizwa kwa siri na mashirika ya kijasusi ya Marekani na Uingereza mwezi Machi 2009.
Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria, Ghana, Sierra Leone, Togo, Guinea Conakry na Sudan.
Kuanzia mwaka 2013 Edward Snowden aliamua kufichua siri za mashirika ya kijasusi ya Marekani baada ya kukerwa na jinsi mashirika hayo yanavyowafanyia ujasusi watu na hata viongozi wakuu wa nchi mbalimbali duniani.