Uchaguzi wa Rais Somalia kufanyika Disemba 28
Viongozi wa kisiasa nchini Somalia wametangaza tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo baada ya kuuakhirisha mara tatu sasa.
Taarifa kutoka Mogadishu zinasema kuwa, viongozi wa kisiasa Somalia wameafikiana kuwa uchaguzi wa rais ufanyike Disemba 28 ambapo inatarajiwa kwanza bunge jipya litamchagua spika tarehe 22 Disemba na kisha baada ya hapo atasimamia zoezi la wabunge kumchagua rais.
Rais wa Somalia hachaguliwi kwa kura ya moja kwa moja na wajumbe 14,000 wa koo mbali mbali huwachagua wabunge takribani 329 ambao nao humachagua rais..
Uchaguzi wa bunge somalia umegubikwa na mizozo mingi yakiwemo madai ya rushwa na wizi wa kura.

Mwezi Agosti mwaka huu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilionyesha masikitiko yake makubwa juu ya mwenendo wa ucheleweshaji wa uchaguzi huo na kuitaka serikali ya Mogadishu kuainisha tarehe mpya kwa ajili ya zoezi hilo muhimu.
Kabla ya hapo pia Michael Keating mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia alisema kuwa, uakhirishwaji uchaguzi huo, utaiongezea jamii ya kimataifa wasi wasi juu ya usalama wake.
Somalia ambayo inafanya juhudi za kukarabati uharibifu wa miongo kadhaa iliyopita, inakabiliwa na mashambulizi ya wanamgambo wa kundi hatari la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab.