Kiongozi wa upinzani ashinda uchaguzi wa rais Ghana, Mahama akubali matokeo
Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Ghana, Nana Akufo-Addo, ameibuka mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Jumatano iliyopita na kumshinda Rais wa sasa John Dramani Mahama.
Jana Ijumaa, Tume ya Uchaguzi ya Ghana ilitangaza kuwa, Akufo-Addo amepata asilimia 53.8 ya kura na kumbwaga Rais Dramani Mahama, aliyezoa asilimia 44.4 ya kura zote. Televisheni ya Taifa ya Ghana GTV imetangaza kuwa, Mahama sambamba na kukubali matokeo, amempigia simu Rais mteule Akufo-Addo na kumpongeza kwa ushindi wake.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ghana, wananchi karibu milioni 16 wameshiriki katika uchaguzi huo wa Rais na Bunge. Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo pia imetangaza kuwa waangalizi wa nchi za nje zaidi ya 400 na elfu 12 wa ndani wamesimamia mchakato wa uchaguzi.
Mahama ambaye alishika hatamu za kuiongoza nchi hiyo Julai mwaka 2012 baada ya kuaga dunia Rais John Atta Mills na kisha kushinda katika uchaguzi mdogo wa 2013, amebwagwa na Nana Akufo-Addo wa chama cha New Patriotic NPP, ambaye alikuwa anawania kiti cha urais kwa mara ya tatu.
Ghana ni moja ya nchi chache za Afrika zenye kuheshimu misingi ya demokrasia na zenye historia ya kushuhudia mchakato wa amani wa kukabidhi madaraka kutoka serikali moja hadi nyingine.