Wapinzani Burundi wamkataa mpatanishi wa mgogoro wa nchi hiyo
Makundi ya upinzani nchini Burundi yamemtaka Benjamin Mkapa, mpatanishi wa kimataifa katika mgogoro wa nchi hiyo ajiuzulu ikiwa ni siku kadhaa zimepita tangu awasili nchini humo na hivyo kuzusha wasiwasi wa kufanikiwa juhudi zinazosuasua za kutatua mgogoro wa machafuko ya kisiasa yanayoendelea kwa miezi kadhaa sasa katika nchi hiyo.
Mkapa aliwasili nchini Burundi siku ya Ijumaa akiongoza ujumbe wa upatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo akiwa katika uwanja wa ndege wa Bujumbura alitoa matamshi ambayo makundi yanayoipinga serikali yanasema yanaashiria kuipa uhalali wa kisheria serikali ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza, suala ambalo ndio kiini cha mgogoro uliopo.
Mrengo mkuu wa muungano wa upinzani wa CNARED jana ulimwandikia barua rais huyo mstaafu wa Tanzania kumtaka aondoke.
Sehemu moja ya barua hiyo imeeleza kuwa: "CNARED haikutambui tena wewe kama mpatanishi katika mgogoro wa ndani wa Burundi".
Alipozungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Bujumbura, Mkapa alisema kipaumbele chake ni kuhakikisha uchaguzi ujao wa rais wa mwaka 2020 unakuwa huru na wa haki.
"Ni watu wa Burundi ndio waliompa uhalali wa kisheria rais wa Burundi... wale wanaodhani mimi ndiye ninayetoa uhalali wa kisheria hawajifahamu hata kidogo", alisema mpatanishi huyo wa EAC.
Burundi imekumbwa na mgogoro wa kisiasa na machafuko ya umwagaji damu kwa muda wa takribani miaka miwili sasa uliochochewa na uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu na kuibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika Julai mwaka uliopita wa 2015, hatua ambayo ilishadidisha zaidi mgogoro huo.../