WHO: Boko Haram imeharibu vituo vya Afya kaskazini mwa Nigeria
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, kundi la kigaidi la Boko Haram limeharibu sehemu kubwa ya vituo vya afya katika eneo la kaskazini mwa Nigeria.
Taarifa iliyotolewa na WHO imesema kuwa, thuluthi moja ya vituo vya afya vya jimbo la Borno huko kaskazini mashariki mwa Nigeria imeharibiwa katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Taarifa jiyo imesema kuwa kundi la kigaidi la Boko Haram ndilo lililohusika na uharibifu huo.
Kundi hilo la kiwahabi lilijitangaza kwa mara ya kwanza mwaka 2002 katika eneo la Maiduguri huko kaskazini mashariki mwa Nigeria na takwimu zinasema, hadi sasa limeua zaidi ya watu elfu 20 na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Siku chache zilizopita Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika ya Kati, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, licha ya kuwa magaidi hao wamekimbia eneo la Ziwa Chad baada ya kufurushwa na kikosi cha askari wa nchi za kanda hiyo, lakini kundi hilo la kigaidi bado ni tishio kwa usalama wa eneo hilo.