Wapizani Kongo DR wasema hawataandamana dhidi ya serikali
Viongozi wa upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesema hawatafanya maandamano kesho Jumatatu dhidi ya serikali, licha ya muhula wa Rais Joseph Kabila kumalizika.
Mkuu wa upinzani Mzee Etienne Tshisekedi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wapinzani hawatafanya maandamano Jumatatu na Jumanne kama ilivyotazamiwa, ili kuepusha maafa na umwagikaji wa damu nchini humo. Amesema: "Hatutaki kutoa mwanya kwa maafisa usalama kuwamininia risasi wananchi na tunawataka wafuasi wetu wawe watulivu na kila mmoja afanye maandamano kivyake, kulalamikia hatua ya Kabila ya kung'ang'ania madaraka."
Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo ya kujaribu kuutafutia ufumbuzi mzozo wa kisiasa nchini DRC yamesitishwa kwa muda. Marcel Utembi, Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki wanaosimamia mazungumzo hayo amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mazungumzo hayo yamesitishwa na yanatazamiwa kuendelea siku ya Jumatano. Mazungumzo hayo yaliyoanza Disemba 8 yalitazamiwa yamalizike Ijumaa ya juzi, lakini yaliakhirishwa hadi jana baada kutofikiwa muafaka na muungano mkuu wa upinzani unaoongozwa na Mzee Tshisekedi.
Umoja wa Mataifa umebainisha wasiwasi wake kufuatia kutangazwa mpango wa serikali ya Kongo DR wa kufunga mitandao ya kijamii kuanzia leo saa sita usiku, wakati muhula wa kuhudumu Rais Kabila kwa mujibu wa sheria utakapomalizika rasmi.
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein amesema hatua hiyo ya DRC inayoenda sambamba na marufuku ya maandamano ya mashirika ya kiraia na vyama vya upinzani, itatekelezwa katika mkesha wa siku ambayo ni ya mwisho kwa Rais Joseph Kabila kuweko madarakani kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.