Watu kadhaa wajeruhiwa katika shambulio la kigaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria
Watu kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio la kigaidi linalosadikiwa kufanywa na wanamgambo wa kundi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Victor Ezwugu msemaji wa jeshi la Nigeria amearifu kuwa mabinti wawili walilipua mikanda ya mabomu waliyokuwa wamejifunga katika kituo kimoja cha upekuzi katika mji wa Maiduguri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Ezwugu ameeleza kuwa, kundi la Boko Haram ndilo lililohusika na shambulio hilo la kigaidi kwa kuzingatia kwamba kundi hilo mara kwa mara huwatumia wanawake na mabinti kujilipua. Mji wa Maiduguri wiki kadhaa zilizopita pia ulikumbwa na mashambulizi kadhaa ya milipuko ya mabomu.
Maafisa usalama wa Nigeria wana wasiwasi kwamba watekelezaji wa mashambulizi hayo ya kigaidi ni pamoja na maelfu ya wanawake na mabinti ambao walitekwa nyara na Boko Haram miaka kadhaa iliyopita.