Wapinzani DRC watoa sharti la kukubali muafaka wa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22039-wapinzani_drc_watoa_sharti_la_kukubali_muafaka_wa_kisiasa
Wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoa sharti ambalo wanasema lazima upande wa serikali ulikubali ili waunge mkono muafaka hafifu wa kisiasa uliofikiwa jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 24, 2016 04:15 UTC
  • Wapinzani DRC watoa sharti la kukubali muafaka wa kisiasa

Wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoa sharti ambalo wanasema lazima upande wa serikali ulikubali ili waunge mkono muafaka hafifu wa kisiasa uliofikiwa jana.

Valentin Mubake, mshauri wa kinara wa upinzani nchini humo, Mzee Etienne Tshisekedi amesema iwapo Rais Joseph Kabila atakubali kung'atuka uongozini mwezi Novemba mwaka ujao 2017, basi wapinzani wataunga mkono kikamilifu makubaliano hayo yaliyofikiwa baada ya mazungumzo ya siku kadhaa, yaliyosimamiwa na Kanisa Katoliki.

Amesema Kabila anafaa kuondoka madarakani muda huo ili kuruhusu anga nzuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki mwishoni mwa mwaka ujao 2017.

Rais Joseph Kabila wa DRC

Martin Fayulu, mmoja wa viongozi wa upinzani Kongo DR ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kwa mujibu wa makubaliano hayo, Rais Kabila ambaye muhula wake wa uongozi kikatiba ulimalizika Disemba 20, atasalia mamlakani hadi mwishoni mwa mwaka ujao wa 2017, ambapo uchaguzi mkuu utaandaliwa. Aidha imeafikiwa kuwa mrengo wa upinzani utamteua Waziri Mkuu mpya, mchakato ambao utasimamiwa kwa karibu na Tshisekedi ambaye pia atasimamia utekelezwaji wa makubaliano hayo.

Kadhalika makubaliano hayo yamebainisha kuwa, katiba ya nchi haitofanyiwa marekebisho kama ilivyokuwa imependekezwa awali na chama tawala kama ambavyo Rais Joseph Kabila hatoruhusiwa kugombea tena kiti cha rais baada ya kuongoza kwa mwaka mmoja.

Ghasia na maandamano ya wapinzani mjini Kinshasa

Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umesema kuwa, zaidi ya watu 40 wameuawa katika ghasia na maandamano ya wananchi ya kushinikiza Rais Kabila aachie ngazi. Hayo yamesemwa na Zeid Ra'ad al-Hussein, Kaimishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ambaye ameongeza kuwa, watu 460 wamekamatwa na maafisa usalama kwa kushiriki maandamano hayo, yaliyopigwa marufuku na serikali ya Kinshasa.