Hofu yatanda Tunisia baada ya magaidi kurejea wakitokea Iraq, Syria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22135-hofu_yatanda_tunisia_baada_ya_magaidi_kurejea_wakitokea_iraq_syria
Maafisa wa usalama nchini Tunisia wameeleza hofu yao kutokana na kuanza kurejea nchini humo maelfu ya magaidi wakufurishaji wanaokimbia kutoka Syria na Iraq baada ya kutimuliwa na majeshi ya nchi hizo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 26, 2016 00:59 UTC
  • Hofu yatanda Tunisia baada ya magaidi kurejea wakitokea Iraq, Syria

Maafisa wa usalama nchini Tunisia wameeleza hofu yao kutokana na kuanza kurejea nchini humo maelfu ya magaidi wakufurishaji wanaokimbia kutoka Syria na Iraq baada ya kutimuliwa na majeshi ya nchi hizo.

Taarifa iliyotolewa Jumapili na Jumuiya ya Kitaifa ya Vikosi vya Usalama wa Ndani imesema: "Kurejea magaidi nchini Tunisia kutoka maeneo ya vita ni jambo linalotia wasiwasi na yumkini nchi hii ikawa kama Somalia."

Taarifa hiyo imesema, magaidi hao sugu wamepata mafunzo ya kijeshi na uwezo wa kutumia silaha za kisasa.

Tahadhari hiyo imetolewa siku moja baada ya maafisa wa usalama wa Tunisia kuwakamatwa washukiwa watatu, akiwemo mjomba wake Anis Amri, mtuhumiwa mkuu wa hujuma ya kigaidi ya tarehe 19 Disemba mjini Berlin, Ujerumani katika soko la Krismasi.

Mapema mwezi huu, Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia alisema katu hatatoa msamaha kwa Watunisia ambao wamewahi kupigana katika makundi ya kigaidi. Jumamosi iliyopita Watunisia waliandamana kupinga kauli ya Rais Essebsi kuwa hawezi kuwaruhusu Watunisia, hata magaidi, kurejea nchini humo.

Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia

Takribani Watunisia 7,000 wanaripotiwa kuondoka nchini humo tokea mwaka 2011 na kujiunga na makundi ya kigaidi yanayowakufurisha Waislamu hasa kundi la Daesh katika nchi za Syria na Iraq.

Hadi sasa magaidi nchini Tunisia wamefanya hujuma kadhaa ambazo ziliwalenga watalii. Utalii ni tegemeo la pato la kigeni kwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.