Tanzania kuchunguza madai ya kuifanyia ujasusi Malawi
Serikali ya Tanzania imesema, itafanya uchunguzi kuhusu habari zilizoripotiwa jana na vyombo vya habari vya Malawi vinavyodai kuwa majasusi wanane wa Tanzania wametiwa mbaroni wakifanya ujasusi katika mgodi mmoja wa urani katika nchi hiyo jirani.
Gazeti la kila siku la The Citizen la nchini Tanzania limeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, taarifa za kutiwa mbaroni watu hao ziliripotiwa kwa mara ya kwanza siku ya Alkhamisi, na vyombo vya habari vya Malawi vikadai jana kuwa, majasusi wanane wametumwa na serikali ya Tanzania kwenda kuchunguza iwapo Malawi inaunda silaha za nyuklia kwa kutumia urani kwenye mgodi wa Kayerekera ulioko katika wilaya ya Karonga au la.
Mitandao ya nyasatimes.com, blantyerpost.com na maravipost.com imeripoti habari hiyo na kudai kuwa kundi hilo la Watanzania limeingia nchini Malawi bila ya hati za kusafiria.

Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Afrika Mashariki wa Tanzania, Dk Augustine Mahiga jana aliliambia gazeti la The Citizen kuwa, hana habari kuhusu ripoti hizo na kuahidi kufuatilia.
"Ndio kwanza nasikia habari hii kutoka kwako. Haya ni madai mazito. Nitafuatilia jioni hii. Nitawasiliana na ubalozi wetu Malawi na maafisa wetu wa intelijensia kujua zaidi kuhusu madai hayo. Haya ni madai mazito sana," amesema Dk Mahiga.
Vyombo vya habari vya Malawi vimezinukuu duru za usalama bila ya kutaja majina zikisema kuwa, baadhi ya Watanzania hao wamekamatwa na vifaa vinavyotia wasiwasi zikiwemo kamera zenye uwezo mkubwa wa kupiga picha.

Moja ya duru hizo za usalama za Malawi zimenukuliwa na vyombo hivyo vya habari zikisema: Swali ni kwamba kwa nini Watanzania hao watembelee mgodi wa Urani wa Kayelekera katika mazingira ya kutatanisha na swali jengine ni kwamba kwa nini walikuwa wanashindwa kutoa sababu za kutembelea eneo hilo. Inaonekana serikali ya Tanzania inadhani kwamba Malawi inajiandaa kufanya kitu kikubwa na ndio maana inafanya kila iwezalo kuchukua tahadhari.
Ikumbukwe kuwa nchi mbili za Tanzania na Malawi zina mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa.
Polisi wa Malawi wamesema, wakazi wa kijiji cha Kayuni walishangazwa walipowaona Watanzania hao wanazunguka zunguka kwenye mgodi huo, na walipoulizwa wanatafuta nini kwenye mgodi huo walishindwa kutoa majibu ya kuridhisha.

Hata hivyo, naibu msemaji wa polisi wa wilaya ya Karonga nchini Malawi, George Mlewa amekanusha madai hayo na kusema wanawashikilia Watanzania hao kwa kosa la kuingia Malawi kinyume cha sheria.
Watanzania hao wametolewa mikononi mwa polisi na kupelekwa katika jela ya Mzuzu.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Malawi, kundi jingine la wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Tanzania waliokwenda Malawi chini ya mwavuli wa Kanisa la Moravian walizuiwa kutembelea mgodi huo ambao hivi sasa umefungwa.