Hatimaye Kongo DR yafikia muafaka wa kisiasa, Kabila kuachia madaraka 2017
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22486-hatimaye_kongo_dr_yafikia_muafaka_wa_kisiasa_kabila_kuachia_madaraka_2017
Hatimaye serikali na upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimefikia muafaka, ambapo Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo amekubali kung'atuka uongozini mwishoni mwa mwaka ujao 2017.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 31, 2016 04:00 UTC
  • Hatimaye Kongo DR yafikia muafaka wa kisiasa, Kabila kuachia madaraka 2017

Hatimaye serikali na upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimefikia muafaka, ambapo Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo amekubali kung'atuka uongozini mwishoni mwa mwaka ujao 2017.

Muafaka huo ni matunda ya mazungumzo baina ya wawakilishi wa serikali na vyama vya upinzani chini ya upatanishi wa Kanisa Katoliki yaliyofanyika mjini Kinshasa jana Ijumaa, siku moja baada ya wapatanishi hao kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Kabila pamoja na kiongozi mkongwe wa upinzani nchini humo Etienne Tshisekedi kuhisiana na mgogoro huo wa kisiasa.

Kwa mujibu wa hati ya makubaliano hayo, Kabila hatabadilisha katiba kwa lengo la kushiriki katika uchaguzi mkuu mwaka ujao 2017 huku utawala wake wa mihula miwili ambao ulimalizika Disemba 19 ukiongezwa hadi mwishoni mwa mwaka ujao na wala sio Aprili 2018 kama ilivyopendekezwa awali. 

Etienne Tshisekedi, kinara wa upinzani DRC

Marcel Utembi, Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo amesema Rais Kabila ataondoka madarakani mwishoni mwa mwaka ujao, ili kupisha uchaguzi mkuu ambao utafanyika kabla ya kumalizika mwaka huo, mbali na kuteua Waziri Mkuu kutoka muungano mkuu wa upinzani unaoongozwa na Mzee Tshisekedi.

Muafaka huo unatazamiwa kutiwa saini rasmi leo Jumamosi ingawaje inaarifiwa kuwa Rais Kabila na Tshisekedi hawatatia sahihi wenyewe, na badala yake kazi hiyo itafanywa na wajumbe wao; jambo ambalo linawatia wasi wasi wadadidi wa mambo ambao wanahisi huenda makubaliano hayo yasiheshimiwe wala kuchukuliwa kwa uzito. 

Polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Kinshasa

Kinachosuburiwa kwa sasa ni kuona iwapo pande hasimu za kisiasa nchini DRC zitaheshimu muafaka huo na nchi hiyo ya Kiafrika kurejea katika hali ya amani, utulivu na uthabiti.

Zaidi ya watu 40 wamepoteza maisha katika siku za hivi karibuni, katika maandamano ya kutaka Kabila aondoke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo tokea mwaka 2001 wakati baba yake, Laurent Desire Kabila, alipouawa.