Kiongozi wa Serikali ajiua kwa kusailiwa nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22687-kiongozi_wa_serikali_ajiua_kwa_kusailiwa_nchini_misri
Duru za habari za Misri zimetangaza habari ya kujiua Katibu Mkuu Mstaafu wa Baraza la Serikali ya nchi hiyo baada ya kutiwa mbaroni na maafisa wa Serikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 03, 2017 02:31 UTC
  • Kiongozi wa Serikali ajiua kwa kusailiwa nchini Misri

Duru za habari za Misri zimetangaza habari ya kujiua Katibu Mkuu Mstaafu wa Baraza la Serikali ya nchi hiyo baada ya kutiwa mbaroni na maafisa wa Serikali.

Mtandao wa habari wa al Yaum al Sabií wa Misri umeripoti habari hiyo ukimnukuu wakili wa Wael al Shalbi, Katibu Mkuu aliyelazimishwa kujiuzulu wa Baraza la Serikali ya Misri akisema kuwa, mteja wake huyo hakuwa katika hali nzuri hata kidogo wakati alipokuwa anasailiwa na alitishia kuwa atajinyonga kama ataendelea kusailiwa. Wakili huyo amesema, kulifanyika juhudi kubwa za kuzuia kujiua al Shalbi lakini juhudi hizo zimeshindikana na jana asubuhi (Jumatatu) alipatikana akiwa amejiua katika korokoro alikokuwa anashikiliwa.

Mwanasheria Mkuu wa Masuala ya Usalama wa Misri alitoa amri ya kutiwa mbaroni al Shalbi kwa tuhuma za kupokea rushwa katika kashfa kubwa iliyoikumba Misri inayojulikana kwa jina la "Rushwa Kubwa" pamoja na mkuu wa kitengo cha manunuzi cha Baraza la Serikali ya Misri na wamiliki wawili wa mashirika binafsi.

 

Wael al Shalbi alipatikana na hatia ya kuhusika kwenye kashfa hiyo kubwa. Alizidi kuingia matatani baada ya nyaraka mbalimbali kufanyiwa uchunguzi na kuonekana anahusika moja kwa moja na kashfa hiyo.

Wael al Shalbi ambaye pia alikuwa jaji maarufu nchini Misri, juzi Jumapili alilazimika kujiuzulu nafasi yake ya Ukatibu Mkuu wa Baraza la Serikali ya nchi hiyo wadhifa ambao aliushikilia kwa muda wa miezi 18, na baadaye kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kula rushwa.