Kuendelea mgogoro wa Ivory Coast
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23248-kuendelea_mgogoro_wa_ivory_coast
Kufuatia mivutano ya kisiasa na kiusalama ya hivi karibuni nchini Ivory Coast Rais Alassane Ouattara wa nchi hiyo amewafuta kazi wakuu wa jeshi na polisi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 11, 2017 05:02 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa Ivory Coast

Kufuatia mivutano ya kisiasa na kiusalama ya hivi karibuni nchini Ivory Coast Rais Alassane Ouattara wa nchi hiyo amewafuta kazi wakuu wa jeshi na polisi ya nchi hiyo.

Katika taarifa Rais Alassane Ouattara amemteua Soumaila Bakayoko kuwa kamanda mkuu mpya wa jeshi akichukua nafasi ya Sékou Touré. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Ouattara pia amewafuta kazi Gervais Kouassi, mkuu wa askari usalama na Brindou Mbia mkuu wa polisi na kwa utaratibu nafasi zao kupewa Nicolas Kouakou na Youssouf Kouyaté.

Mabadiliko hayo yanafuatia uasi ambao ulifanywa wiki iliyopita  na wanajeshi ambao walitishia usalama wa taifa hilo. Wanajeshi hao waliteka na kudhibiti kwa muda kambi za jeshi katika miji mitano ya nchi hiyo wakitaka matakwa yao kuhusu mishahara na hali yao ya maisha yashughulikiwe kwa haraka. Kufuatia hali hiyo Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo aliamua kutuliza hali ya mambo kwa kukutana na skari jeshi hao waasi kwa lengo la kujadiliana nao kuhusu utatuzi wa matatizo yao lakini wakaamua kumteka nyara.

Rais Alassane Uoattara

Hata hivyo hali hiyo ilitatuliwa kwa ahadi za Rais Ouattara ambaye aliahidi kuwaongezea mishahara na kushughulikia suala la makazi yao, jambo ambalo liliwatuliza na hivyo kumuachilia huru waziri huyo wa ulinzi. Lakini ikiwa ni siku chache tu zimepita tokea kujiri kwa ausi huo wa wanajeshi Rais Ouattara amewashangaza wengi kwa kuamua kuwafukuza kazi makamanda wa jeshi, askari usalama na polisi. Inaonekana kuwa Ouattara ameamua kuchukua uamuzi huo ili kuimarisha usalama wa taifa na kuepusha kutokea  uasi mwingine kama huo na mapinduzi ya kijeshi chini. Wakati huohuo Waziri Mkuu wa nchi hiyo pia amejiuzulu na serikali yake kuvunjiliwa mbali. Hata kama kuvunjwa serikali ni jambo lililokuwa likitarajiwa hasa baada ya kupitishwa katiba mpya ya nchi hiyo lakini Waziri Mkuu amewasilisha ombi lake la kujiuzulu mara tu baada ya kujiri uasi huo wa wanajeshi. Hata kabla ya Uoattara kuchukua uamuzi kuhusiana na ombi hilo tayari mgomo wa wafanyakazi wa serikali umeanza kote nchini humo. Wengi wa wafanyakazi hao ni wapinzani wakubwa wa Rais Ouattara na waungaji mkono wa rais wa zamani wa nchi hiyo. Wafanyakazi hao wanadai kuongezewa mishahara.

Waziri wa Ulinzi wa Ivory Coast (katikati) akiwa ametekwa nyara na wanajeshi waasi

Ni wazi kuwa mgomo huo utakuwa na athari kubwa kwa sekta ya elimu na afya nchini. Hii ni katika hali ambayo katika kampeni zake za kuwania duru ya pili ya urais wa Ivory Coast, Ouattara aliahidi kuimarisha umoja wa kitaifa, kulinda sheria, kuheshimu haki za binadamu na kulinda usalama wa taifa. Aliahidi pia kuimarisha hali ya maisha na uchumi wa nchi hiyo ahadi ambayo hajaitekeleza hadi sasa. Hali ya Ivory Coast inaedelea kuvurugika katika hali ambayo askari wa kulinda usalama walioko nchini humo wanajiandaa kuondoka mwezi Juni ujao. Askari hao wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walitumwa nchini humo kufuatia mgogoro wa kisiasa na mauaji ya umati yaliyozuka nchini humo miaka kadhaa iliyopita. Tayari majukumu yaliyokuwa yametwishwa ujumbe wa kimataifa nchini humo sasa yamekabidhiwa serikali ya Uoattara.

Wanajeshi waasi wakipiga doria katika baadhi ya miji ya Ivory Coast

Licha ya kuwa kukabidhiwa huko kwa majukumu ya serikali kunaonyesha kuimarika hali ya kisiasa na kiusalama nchini lakini mivutano ya hivi sasa imezua tena wasiwasi katika ngazi za kitaifa na kimataifa kuhusu jambo hilo. Hata kama mabadiliko hayo ambayo yamefanywa na Rais Ouattara yanalenga kuimarisha usalama na uthabiti wa kisiasa lakini ni wazi kuwa usalama na utulivu wa kudumu utarejeshwa nchini pale tu matakwa muhimu ya wananchi yatakapotekelezwa na serikali. Kuboreshwa kwa hali ya ajira, nyongeza ya mishahara, kutekelezwa uadilifu na kulindwa usalama pamoja na kuheshimiwa haki za binadamu ni miongoni mwa matakwa hayo muhimu ya wananchi wa Ivory Coast.