Jan 13, 2017 07:32 UTC
  • Rais Teshome atoa wito wa kuimarishwa uhusiano wa Ethiopia na Iran

Rais Mulatu Teshome wa Ethiopia amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili kati ya Tehran na Addis Ababa.

Matamshi hayo yametolewa katika ujumbe uliotumwa na Rais wa Ethiopia kwa mwenzake wa Iran, Dakta Hassan Rouhani kwa mnasaba wa kifo cha rais wa zamani wa Iran Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani.

Rais wa Ethiopia amesema kwa niaba ya nchi yake, anatoa salamu za rambirambi kwa taifa na serikali ya Iran kutokana na kifo cha Ayatullah Rafsanjani, aliyefariki dunia siku chache zilizopita.

Marehemu Ayatullah Rafsanjani

Mbali na kutoa mkono wa pole kufuatia kifo cha shakhsia huyo wa Iran, Rais Mulatu Teshome wa Ethiopia amesema nchi yake iko tayari kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili na Iran katika nyuga mbalimbali.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kwa mara imekuwa ikisitiza kuwa, sera zake za mambo ya nje zinatoa kipaumbele katika suala la kuimarishwa uhusiano na nchi za bara Afrika. 

Salamu za rambirambi zimeendelea kutolewa na viongozi na shakhsia mbalimbali duniani kufuatia kifo cha Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran marehemu Sheikh Rafsanjani.

Ayatullah Rafsanjani aliaga dunia Jumapili iliyopita kutokana na matatizo ya moyo katika hospitali moja ya mjini Tehran na mwili wake ukazikwa pambizoni mwa kaburi la mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini katika eneo al Behest Zahraa, kusini mwa Tehran.

Tags