Chuki dhidi ya Uislamu, chanzo cha kuhujumiwa misikiti Afrika Kusini
Serikali ya Afrika Kusini imesema chuki dhidi ya Uislamu ndio chanzo cha hujumza mbili dhidi ya misikiti mjini Cape Town.
Katika taarifa, serikali ya eneo la Cape Magharibi imeashiria matukio ya hivi karibuni ambapo damu ilipakwa katika kuta za msikiti Kalk Bay na hujuma nyingine ya msikiti wa Simon Town ambapo pua la nguruwe liliwekwa msikitini na kusema, "matukio hayo mawili ni njama ya makusudi ya chuki dhidi ya Uislamu." Taarifa hiyo imesema kwa kuzingatia kushabihiana vitendo hivyo viwili na kukaribiana misikiti iliyolengwa kuna wasi wasi kuwa vitendo hivyo viwili vinahusiana."
Sheikh Achma Sity, Imamu wa Msikiti wa Kalk Bay uliojengwa miaka 110 iliyopita ametoa wito kwa Waislamu kuwa watulivu na kudumisha umoja.
"Msikiti huu umekuwepo hapa kwa zaidi ya miaka 100 na ni mara ya kwanza kwa tukio kama hilo kujiri," amemwambia mwandisi wa Al Jazeera.
Tawi la chama tawala cha ANC katika eneo hilo limelaani hujuma hiyo na kuitaja kuwa ya "kuchukiza" sambamba na kutoa wito kwa watu wa Afrika Kusini kudumisha umoja na kulinda utamaduni wa kustahamiliana.
Farid Sayed, mhariri wa jarida la Muslim Views amesema hujuma hizo zinaashiria kuwa baadhi ya watu wameshindwa kujiunga na jamii nzima baada ya mfumo wa ubaguzi wa rangi kupinduliwa Afrika Kusini.
Amesema vyombo vya habari vya mrengo wa kulia vinachochea hisia za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Kati ya watu 55 milioni nchini Afrika Kusini asilimia 1.5 ni Waislamu na wengi wana nafasi muhimu za kisiasa, katika vyuo vikuu, biashara n.k.