Tunisia na tatizo la kurejea magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23746-tunisia_na_tatizo_la_kurejea_magaidi
Kurejea katika nchi zao magaidi waliojiunga na makundi ya kigaidi lingali miongoni mwa matatizo na changamoto kubwa ambazo ni gumzo barani Ulaya na Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 17, 2017 09:41 UTC
  • Tunisia na tatizo la kurejea magaidi

Kurejea katika nchi zao magaidi waliojiunga na makundi ya kigaidi lingali miongoni mwa matatizo na changamoto kubwa ambazo ni gumzo barani Ulaya na Afrika.

Nchi nyingi za Ulaya zina wahaka na wasiwasi wa kurejea raia wake ambao walijiunga na makundi yenye kufurutu ada na kwa sasa zinatafuta njia na mikakati ya kukabiliana na kurejea magaidi katika nchi zao. Barani Afrika nako wasiwasi huo umegeuka kuwa tatizo kuu hususan kwa nchi kama Tunisia.

Filihali, serikali ya Tunisia haikabiliwi tu na tishio la ugaidi mipakani kutokana na kupakana na nchi kama Libya na eneo la Sahel na makundi ya kigaidi ya dhahiri na ya siri, bali inakabiliwa pia na hatari kubwa ya kurejea nchini humo raia wa nchi hiyo waliojiunga na makundi ya kigaidi.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh

Ripoti zinaonesha kuwa, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, raia takribani 6,000 hadi 10,000 wa Tunisia walijiunga katika safu ya makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi za Syria, Iraq na Libya. Baadhi ya wanachama wa makundi hayo ya kigaidi wameuawa nje ya Tunisia huku 2,000 kati yao wakiwa katika orodha ya waliotoweka bila kujulikana hatima yao. Hata hivyo kuna wengine wengi ambao ama wamerejea  nchini Tunisia au wamo mbioni kurejea katika nchi yao. Hivi sasa kutokana na kushindwa magaidi katika akthari ya maeneo ya Syria na Iraq, mwenendo wa kurejea makwao magaidi hao umechukua kasi zaidi.

Mwanzoni mwa mwaka huu huu, maelfu ya Watunisia walijitokeza katika barabara za nchi hiyo ambapo mbali na kuandamana wakipinga hatua ya kurejea nchini humo raia wa nchi hiyo waliojiunga na makundi ya kigaidi, waliitaka serikali ya Tunis izuie magaidi hao kurejea nchini humo. Pamoja na kuwa, hapo kabla baadhi ya viongozi wa Tunisia walizungumzia uwezekano wa kusamehewa raia wa nchi hiyo waliojiunga na makundi ya kigaidi endapo watatubia, lakini malalamiko ya wananchi yaliwafanya viongozi wa Tunis wabadilishe msimamo na kuahidi kuwatia mbaroni magaidi hao mara watakaporejea, hatua ambayo ililenga kupunguza wasiwasi uliopo wa kurejea wanachama hao wa makundi ya kigaidi. Viongozi wa Tunisia waliahidi kwamba, wanachama wa makundi ya kigaidi wanaorejea nchini humo watatiwa mbaroni na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya kupambana na ugaidi.

Bendera ya Tunisia

Akthari ya wananchi wa Tunisia wanaamini kuwa, kurejea nchini humo raia wa nchi hiyo waliojiunga na makundi ya kigaidi ni tishio la kweli kwa usalama wa taifa wa nchi yao na ndio maana baadhi yao wamekwenda mbali zaidi na kutaka magaidi hao wapokonywe uraia wa nchi hiyo. Hata hivyo viongozi wa Tunis wanasema kuwa, kufanya hivyo ni kinyume na sheria za nchi na ndio maana wanasema kuwa, wahusika hao wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Katika upande mwingine kuna ripoti zinazoonyesha kuwa, nchi za Ulaya nazo zimeazimia kutowaruhusu kuingia nchini humo raia wake waliojiunga na makundi ya kigaidi au zitawaweka katika kambi maalumu zinazojengwa nje ya mipaka ya nchi hizo. Kwa muktadha huo basi, kuna uwezekano mkubwa magaidi hao wa Ulaya wakawekwa pamoja na wapiganaji wenzao wa nchi kama Tunisia pambizoni mwa mipaka ya nchi hiyo.

Kikosi maalumu cha Tunisia kikiwa katika mji wa Ben Gardane

Ndani ya Tunisia kwenyewe pia hatari ya harakati za makundi ya kigaidi pamoja na hujuma na mashambulio yao imevuruga kabisa utulivu na uthabiti wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Mji wa Ben Gardane (Bin Qirdan) wa kusini mashariki mwa Tunisia ambao upo katika jimbo la Medenine unahesabiwa kuwa kitovu cha mgogoro wa usalama nchini Tunisia.

Kutokana na mji huo kupakana na Libya pamoja na kivuko cha mpaka cha Ras Jedir umegeuka kuwa sehemu ya mkusanyiko na harakati za makundi ya kigaidi na kitakfiri na kuhesabiwa kuwa moja ya miji inayolengwa na kundi la kigaidi la Daesh nchini Tunisia.

Katika mwaka uliopita mara kadhaa mji wa Ben Gardane ulishuhudia mapambano baina ya wanachama wa makundi ya kigaidi na kitakfiri na vikosi vya usalama ambapo mapigano yaliyokuwa na umwagaji mkubwa zaidi ni yale ya mwezi Machi mwaka jana ambapo kundi la kigaidi la Daesh lilifanya shambulio katika mji huo na kupelekea watu wapatao 60 kuuawa na kujeruhiwa.

Baadhi ya magaidi wa Kitunisia

Aidha mji wa Sousse ulioko katika pwani ya mashariki ya Tunisia ambao uko jirani na mipaka ya Algeria unahesabiwa kuwa kitovu cha pili muhimu cha mgogoro wa usalama nchini Tunisia. Katika mazingira kama haya, wasiwasi na wahaka wa kurejea magaidi na wao wenyewe kupanga operesheni za kigaidi zitakazovuruga usalama wa Tunisia kwa upande mmoja; na kwa upande wa pili kupenya magaidi hao na kuingia katika nchi nyingine za eneo zenye amani na usalama ikiwemio Algeria, ni miongoni mwa daghadagha kuu ya viongozi wa nchi za eneo hilo.