Juhudi za kufanyika makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani nchini Gambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23818-juhudi_za_kufanyika_makabidhiano_ya_madaraka_kwa_njia_ya_amani_nchini_gambia
Katika kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Gambia, Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo sanjari na kulaani uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo, ametangaza hali ya hatari nchini humo.
(last modified 2026-01-02T07:57:23+00:00 )
Jan 18, 2017 13:31 UTC
  • Juhudi za kufanyika makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani nchini Gambia

Katika kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Gambia, Rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo sanjari na kulaani uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo, ametangaza hali ya hatari nchini humo.

Hatua hiyo ya Rais Jammeh imejiri katika hali ambayo imebakia siku moja kabla ya kuapishwa rais wa nchi hiyo, sherehe ambazo zimepangwa kufanyika Alkhamis ya kesho tarehe 19 Januari. Hadi sasa Jammeh amekataa kukubali matokeo ya uchaguzi na licha ya mazungumzo ya kieneo yenye lengo la kumkinaisha ili akabidhi madaraka kwa njia ya amani, lakini bado anaendelea kusisitiza kusalia madarakani. Rais Jammeh aliingia madarakani, mwaka 1994 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kuendelea kuitawala nchi hiyo kama rais aliyechaguliwa na wananchi kuanzia mwaka 1996. Katika kipindi hicho licha ya kwamba alijitahidi kuimarisha kwa kiasi fulani uthabiti wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo, lakini kukosekana uhuru wa kisiasa na kijamii, kutoheshimiwa haki za binaadamu, utumiaji vitisho na ukatili ni mambo yaliyoandaa malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali yake.

Rais Yahya Jammeh wa Gambia

Ni kwa ajili hiyo ndipo katika uchaguzi uliopita, wapinzani sambamba na kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya mabadiliko ya kisiasa, wakamchagua kiongozi wa upinzani Adama Barrow kuchukua nafasi ya Jammeh. Hata hivyo misuguano ya sasa inayoshuhudiwa nchini Gambia imewazidishia wasi wasi wananchi. Hivi sasa mazungumzo ya kieneo hayajazaa matunda kuhusu usuluhishi wa mgogoro wa Gambia na hivyo kuzidisha anga ya khofu na wasi wasi mkubwa nchini humo. Akthari ya viongozi wa serikali ya Banjul wametangaza kujiuzulu nyadhifa zao huku wengine wakiamua kutoroka nchi. Ni siku moja tu imebaki kabla ya kuapishwa rais huku hatua za Jammeh zikizidisha uwezekano wa kutokea vita na machafuko ya ndani nchini humo.

Adama Barrow akifurahia ushindi wake

Hii ni katika hali ambayo kabla ya hapo asasi za kieneo zilikuwa zimetahadharisha kuhusu uwezekano wa kuzuka machafuko hayo na kusisitiza kuwa hazitaruhusu nchi hiyo itumbukie katika hali ya mchafukoge. Katika mazingira hayo, Gambia imesaliwa na machaguo mawili la kwanza likiwa ni kufanikisha juhudi za mazungumzo yanayoendelea kwa lengo la kumkinaisha Rais Yahya Jammeh akubali rasmi matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita na hivyo kukabidhi madaraka kwa njia ya amani kwa mpinzani wake Adama Barrow ili kuliwezesha taifa hilo listawi kisiasa.

Rais Alassane Ouattara wa Côte d’Ivoire

La pili ni kwamba ikiwa Jammeh ataendelea na msimamo wake wa kung'ang'ania madaraka, bila shaka nchi hiyo itakumbwa na machafuko na hivyo kuvifungulia mlango vikosi vya kieneo kuingia katika taifa hilo na hivyo kuzusha machafuko nchini humo. Katika hali hiyo Gambia itakabiliwa na hatma iliyozikumba nchi kadhaa za Kiafrika, ikiwemo Côte d’Ivoire, ya kuwaondoa kwa nguvu viongozi wanaongángánia madaraka. Nchini Côte d’Ivoire kitendo cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo cha kukataa ushindi wa Alassane Ouattara katika uchaguzi wa mwaka 2010, kiliitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa ambapo kwa akali watu 3,000 waliuawa. Kutoheshimu demokrasia na kufanya njama ya kusalia madarakani ni moja ya matatizo makubwa yanayozikabili nchi nyingi za Kiafrika.

Laurent Gbagbo rais wa zamani wa Côte d’Ivoire

Katika miaka ya hivi karibuni migogoro mingi ya kisiasa imekuwa ikisababishwa na viongozi wengi wa bara hilo kung'ang'ania madaraka. Raia wengi wa nchi za bara la Afrika hawafurahishwi na tabia ya viongozi wao ya kusalia madarakani na ni kwa msingi huo ndio maana wakawa wanasisitizia umuhimu wa kuheshimiwa demokrasia ndani ya mataifa hayo. Katika hali hiyo inatazamiwa kuwa viongozi wa bara la Afrika wataheshimu matakwa ya wananchi kama ambavyo kukubali Rais Jammeh kuondoka madarakani na kukabidhi madaraka kwa njia ya amani, itakuwa ni hatua moja mbele katika kuimarisha demokrasia nchini Gambia.