Kurefushwa muda wa hali ya hatari nchini Tunisia
Rais Muhammad Al-Baji Qaid As-Ssebsi wa Tunisia jana alitangaza kurefushwa sheria ya hali ya hatari nchini humo kwa muda mwingine wa mwezi mmoja. Baada ya kushauriana na Waziri Mkuu Yusuf Ash-Shahid, Rais As-Ssebsi ametangaza kuwa sheria ya hali ya hatari itaendelea kutekelezwa nchi nzima kuanzia tarehe 17 Januari hadi tarehe 15 Februari.
Hali ya hatari nchini Tunisia ilitangazwa mara ya kwanza Januari 14 mwaka 2011. Iitarajiwa kuwa baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo dikteta Zine al-Abidine Ben Ali, kukimbilia Saudi Arabia, zama mpya za Tunisia hazitashuhudia utekelezaji wa sharia ya hali ya hatari, lakini matarajio hayo yalithibiti kwa kipindi kifupi tu.
Hali ya hatari iliyotangazwa nchini Tunisia Januari 2011 iliendelea kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu na kuhatimishwa mwezi Machi mwaka 2014. Sababu ya kuendelea kutekelezwa sheria hiyo kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu ilikuwa ni kuendelea kushuhudiwa machafuko yaliyotokana na fujo zilizofanywa na wafanyakazi wa vibarua, migomo na machafuko katika baadhi ya maeneo ya nchi. Kipindi cha baina ya Machi 2014 hadi Novemba 2015, hakikushuhudia utekelezwaji wa sharia ya hali ya hatari nchini Tunisia, lakini mnamo mwezi Novemba mwaka 2015, Rais Muhammad Al-Baji Qaid As-Ssebsi alitangaza tena sheria hiyo ambayo licha ya kupita miezi 14 tangu wakati huo ingali inaendelea.
Sababu iliyomfanya Rais wa Tunisia atangaze tena hali ya hatari Novemba 2015 ni mripuko uliotokea kwenye basi lililobeba askari wa gadi ya rais. Askari 12 wa usalama waliuawa; na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh likatangaza kuhusika na shambulio hilo. Kurefushwa mara kadhaa sharia ya hali ya hatari kwa muda wa mwezi mmoja au miezi mitatu kulifanyika kutokana na hofu ya kutokea mashambulio ya kigaidi. Na katika kipindi cha karibuni, wasiwasi mkubwa zaidi umetokana na taarifa za kurudi nchini Tunisia magaidi kutoka Syria, Iraq na Libya ambao walikuwa wanachama wa makundi ya kigaidi. Kurudi maelfu ya magaidi wenye uraia wa Tunisia kutoka nchi za Syria, Iraq na Libya imegeuka kuwa kadhia muhimu ya kiusalama na uwanja wa changamoto za kisiasa ndani ya nchi hiyo. Maelfu ya Watunisia wameandamana kutaka magaidi hao wasiruhusiwe kukanyaga tena ardhi ya nchi hiyo, lakini hitilafu za mitazamo zimejitokeza kuhusiana na takwa hilo kati ya mirengo na vyombo mbalimbali vya dola likiwemo bunge la nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo Rais As-Ssebsi amesema hawezi kuwazuia watu hao wasirejee nchini lakini akaongeza kwamba itabidi wawe chini ya udhibiti na uangalizi maalumu. As-Sebsi aidha ametangaza rasmi kuwa kwa mujibu wa katiba ya Tunisia haiwezekani kuwazuia magaidi wasirudi nchini mwao; lakini kama wananchi wote watapinga kurejea magaidi hao ataifanyia mabadiliko katiba hiyo.
Inapasa tuseme kuwa kurefushwa sheria ya hali ya hatari nchini Tunisia kwa kipindi kingine cha mwezi mmoja kuna uhusiano wa moja kwa moja na suala la kurejea nchini humo magaidi raia wa nchi hiyo waliokuwa wakitumikia makundi ya kigaidi katika mataifa mengine. Sheria hiyo ya hali ya hatari inampa mamlaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya kuwalazimisha watu wabaki kwenye makazi maalumu na kutekeleza marufuku ya kutotoka nje bila ya kuhitajia kibali cha mahakama. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa hii si mara ya mwisho kwa sheria ya hali ya hatari kurefushwa nchini Tunisia, bali baada ya kumalizika mwezi mmoja uliowekwa, sheria hiyo itarefushwa tena kwa kipindi kingine…/