Iran na Uganda zasisitiza juu ya kustawisha zaidi ushirikiano baina yao
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uganda zimesisitiza juu ya kustawisha zaidi uhusiano wao katika nyanja mbalimbali.
Hayo yamesisitizwa na balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kampala Uganda alipokutana na kufanya mazungumzo hapo jana na Rebecca Kadaga, Spika wa Bunge la Uganda.
Katika mazungumzo hayo, Sayyid Murteza Murtazavi, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kampala amemkabidhi Spika wa Bunge la Uganda mwaliko wa Spika wa Bunge la Iran wa kufanya safari hapa nchini.
Kwa upande wake Bi Rebecca Kadaga, Spika wa Bunge la Uganda sambamba na kueleza hamu na shauku ya nchi yake ya kustawisha zaidi uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika uga wa mahusiano ya mabunge ya pande mbili, amemshukuru Dakta Ali Larijani Spika wa Bunge la Iran kwa kumwalika kuitembelea Jamhuri ya Kiislamu.
Aidha Spika wa Bunge la Uganda ametoa pongezi kwa Iran kwa kuondolewa vikwazo ikiwa ni natija ya mazungumzo ya nyuklia kati yake na madola sita makubwa duniani na kueleza kwamba, mazingira hayo yanafungua ukurasa mpya ambao unaweza kutumiwa na nchi nyingine kwa ajili ya kupanua ushirikiano na Tehran.
Spika wa Bunge la Uganda amesisitiza pia juu ya uungaji mkono wa Bunge la nchi hiyo kwa makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Tehran na Kampala yenye lengo la kurahisisha uhusiano wa kiuchumi wa pande mbili.