Kulemazwa Ivory Coast na migomo inayoendelea nchini humo
Kuendelea mgogoro nchini Ivory Coast na kuanza migomo ya wafanyakazi wa matabaka mbalimbali kumeifanya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ilemazwe kutokana na kukosekana huduma nyingi kulikosababishwa na kufungwa baadhi ya idara.
Wananchi wenye hasira wa matabaka mbalimbali wa Ivory Coast wakiwa na lengo la kutangaza mfungamano wao na wafanyakazi wa huduma za kijamii za nchi hiyo katika miji mbalimbali, wamemiminika katika mitaa na barabara ili kupaza sauti ya malalamiko dhidi ya serikali. Hii ni katika hali ambayo, wanajeshi wastaafu wa Ivory Coast wamefunga njia kuu kadhaa za miji tofauti ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Aidha walimu wengi wameitisha mgomo hatua ambayo imepelekea shule nyingi kufungwa. Migomo hiyo pia imepiga hodi hadi katika sekta ya kikosi cha Zimamoto. Rais Alassane Ouattara aliahidi kuboresha hali ya uchumi wa nchi hiyo hususan katika uchaguzi wa duru ya pili.
Biashara kubwa nchini Ivory Coast ni uzalishaji na usafirishaji nje ya nchi hiyo zao la kakao. Kubadilika bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia na kuporomoka thamani yake kumeibua matatizo makubwa ya kiuchumi katika nchi hiyo. Ivory Coast ndio nchi ya kwanza duniani kwa uzalishaji wa kakao na zaidi ya asilimia 50 ya usafirishaji bidhaa za nchi hiyo nje ya nchi unadhamini theluthi mbili ya ajira na kipato cha wananchi wa nchi hiyo.
Kwa msingi huo basi, kuporomoka bei ya kakao katika soko la dunia, ni jambo ambalo kama zilivyo nchi nyingine zenye kutegemea zao moja kutatoa pigo kubwa kwa uchumi wa Ivory Coast.
Katika upande mwingine kubadilishwa sheria za kustaafu katika nchi hiyo, kuongezwa ada ya bima kutoka asilimia 6 hadi 8.33, kuongezwa umri wa kustaafu sambamba na kupunguzwa kwa asilimia 30 hadi 50 mishahara ya wafanyakazi wastaafu sio tu kwamba, kumeongeza gharama za maisha, bali kumeibua wimbi kubwa la malalamiko ya kijamii nchini humo.
Malalamiko ya wanajeshi wastaafu nchini Ivory Coast yamezidisha wasiwasi wa kutokea mapinduzi nchini. Kufuatia hilo, Rais Alassane Ouattara aliwauzulu na kuwabadilisha makamanda wengi wa jeshi na kukubali kujiuzulu Waziri Mkuu na baraza lake la mawaziri. Hata kama kuvunjwa serikali ni jambo lililokuwa likitarajiwa hasa baada ya kupitishwa katiba mpya ya nchi hiyo, lakini Waziri Mkuu aliwasilisha ombi lake la kujiuzulu mara tu baada ya kujiri uasi wa wanajeshi.
Hivi sasa katika hali ambayo mivutano inaonekana kuongezeka nchini Ivory Coast baada ya kufanyika uchaguzi wa Rais na Bunge katika mazingira tulivu na ya amani, vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyoko nchini humo, vimo katika hali ya kuondoka katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Katika mazingira kama haya, endapo matakwa ya wananchi ya kuboreshwa hali ya sasa ya uchumi na ya kijamii na kuweko anga ya wazi ya kisiasa hayatatekelezwa; basi bila shaka hatari ya kutokea mapinduzi na kuongezeka malalamiko katika nchi hiyo ni mambo ambayo yataendelea kuinyemelea Ivory Coast.