Serikali Ivory Coast: Mgomo wa wafanyakazi uhitimishwe ili tuimarishe uchumi
Serikali ya Côte d’Ivoire imewataka wafanyakazi wake kuhitimisha mgomo wao mara moja sanjari na kurejea kazini.
Taarifa iliyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano ya nchi hiyo imeutaja mgomo huo kuwa usio wa kisheria na kutishia kuwa, ikiwa wafanyakazi hao wa serikali wataendelea na mgomo basi serikali itasimamisha mazungumzo yanayoendelea kwa ajili ya kutatua tofauti zilizopo. Aidha ripoti hiyo imesema kuwa, kutofika kwenye maeneo ya kazi hususan katika sekta ya elimu ni suala linalokinzana na sheria na lisilokubalika na kwamba serikali imeazimia kuwaondoa wawakilishi wake kwenye meza ya mazungumzo ikiwa hali hiyo itaendelea.
Mgomo wa wafanyakazi wanaodai nyongeza ya mishahara na kulipwa marupurupu yao umezidi kuongezeka nchini humo. Kadhalika wafanyakazi hao wanalalamikia sheria ya kustaafu iliyopitishwa mwaka 2012 na kuanza kutekelezwa mwaka jana wa 2016. Kwa mujibu wa sheria hiyo, umri wa kustaafu utaongezwa kutoka miaka 55 hadi 60. mgomo huo ulianza tarehe tisa mwezi huu.