Somalia yatangaza tarehe mpya ya uchaguzi wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24281-somalia_yatangaza_tarehe_mpya_ya_uchaguzi_wa_rais
Kwa mara nyingine tena Somalia imetangaza tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi wa rais licha ya mji mkuu wa nchi hiyo kutikiswa na shambulizi la kigaidi hapo jana.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 26, 2017 10:14 UTC
  • Somalia yatangaza tarehe mpya ya uchaguzi wa rais

Kwa mara nyingine tena Somalia imetangaza tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi wa rais licha ya mji mkuu wa nchi hiyo kutikiswa na shambulizi la kigaidi hapo jana.

Tume ya Uchaguzi ya Somalia imetangaza Februari 8 kuwa tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi wa rais ambao umesubiriwa kwa hamu na shauku kuu.

Watu 83 wameripotiwa kuuawa katika shambulizi la kigaidi lililotekelezwa jana na wanachama wa genge la ash-Shabab, katika lango la kuingilia katika hoteli ya Dayah, karibu na bunge na ikulu ya rais wa Somalia; shambulizi ambalo limetajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kufanyika tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017.

Athari za hujuma ya kigaidi ya jana Mogadishu

Tarehe mpya ya uchaguzi wa rais Somalia imeafikiwa baada ya mazungumzo ya kina baina ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi na bunge jipya la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, ambalo wabunge wake waliapishwa mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba.

Mapema mwezi jana, viongozi wa kisiasa nchini Somalia walitangaza Disemba 28 kuwa tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo baada ya kuuakhirisha mara tatu.

Rais wa Somalia hachaguliwi kwa kura ya moja kwa moja ya wananchi. Wajumbe 14,000 wa koo mbali mbali huwachagua wajumbe 329 wa Bunge la Federali la nchi hiyo ambao nao humchagua rais.