Kiongozi wa kundi la al Shabab auawa Somalia
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa vyombo vya usalama nchini Somalia ametangaza habari ya kuuliwa mmoja wa viongozi wa kundi la kigaidi la wanamgambo wa al Shabab nchini humo.
Iman Karashe amesema kuwa, Abdallah Ghanas mmoja kati ya vinara wa kundi la al Shabab ameuawa katika eneo la Juba ya Kati kusini mwa Somalia katika mapigano yaliyojiri kati ya wanajeshi wa serikali na kundi hilo.
Iman Karashe amesema kuwa oparesheni ya jeshi la Somalia na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika huko Somalia (AMISOM) dhidi ya wanamgambo wa al Shabab inaendelea kwa nguvu zote.
Katika upande mwingine, Fransisco Madeira, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia amesema kuwa kikosi cha AMISOM kimepata mafanikio makubwa nchini humo kwa kushirikiana na wanajeshi wa serikali katika kurejesha amani, tangu kikosi hicho kitumwe nchini humo mwaka 2007.
Hadi kufikia sasa wanajeshi wa AMISOM wamepata mafanikio makubwa katika kudhamini usalama nchini Somlia. Hata hivyo kundi la kigaidi la al Shabab lingali linaendeleza mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Kundi hilo ambalo lina mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida linahusika katika mashambulizi ya umwagaji damu katika nchi za Somalia, Kenya na Uganda.