Mar 05, 2016 15:13 UTC
  • Taasisi za kimataifa zakaribisha kuidhinishwa matokeo ya uchaguzi wa CAR

Taasisi za kimataifa zimekaribisha hatua ya kuidhinishwa Rais mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Katikati mwa Afrika na vile vile Umoja wa Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (Francofone) zimetoa taarifa ya pamoja zikiunga mkono kuidhinishwa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Taasisi hizo za Kimataifa zimesema kuwa zinaunga mkono kurejeshwa amani na kufikiwa mapatano ya kitaifa nchini humo. Wakati huo huo taasisi hizo zimewapongeza viongozi wa serikali ya mpito ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na juhudi zao za kurejesha amani ya kudumu na ustawi wa kiuchumi na kijamii nchini humo.

Taarifa ya pamoja ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na jumuiya ya Francophone imeongeza kuwa taasisi za kimataifa ziko tayari kikamilifu kuisadia serikali mpya ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mahakama ya katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imeidhinisha ushindi wa Rais mpya wa nchi hiyo, Faustine Archange Touadera kupitia uchaguzi wa rais wa Februari 14 mwaka huu na kupinga ombi la aina yoyotla vyama vya upinzani la kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo.

Tags