Mar 06, 2016 02:39 UTC
  • Magaidi wa ISISI wanaenea kwa kasi ya kuogofya Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa magaidi wakufurishaji wa Daesh wanaenea kwa kasi ya kuogofya nchini Libya.

Akizungumza akiwa nchini Mauritania, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu wahusika walio nje ya Libya ambao wanachochea mgogoro nchini humo.

Ban ambaye aliondoka Mauritania Jumamosi akielekea Aligeria kama sehemu ya safari yake ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika, amesema taathira za mgogoro wa Libya zinahisika nje ya mipaka ya nchi hiyo. Amesema mafanikio katika kurejesha amani Libya yatakuwa na faida kwa eneo zima la Sahel barani Afrika na dunia nzima kwa ujumla.

Libya ilitumbukia katika ghasia na machafuko ya ndani baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta wa Muammar Gaddafi mwaka 2011. Maeneo kadhaa ya nchi hiyo kwa sasa yanadhibitiwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh.

Hadi sasa serikali ya umoja wa kitaifa haijaundwa nchini humo kutokana na mivutano iliyopo kati ya makundi tofauti ya kisiasa.

Tags