UNICEF: Watoto Waafrika wavukao Mediteranea kuelekea Ulaya wanateswa vibaya
Safari ya watoto wanaokimbia mizozo na mateso Afrika kwenda Ulaya kupitia bahari ya Mediteranea imegubikwa na mateso ikiwemo ukatili wa kingono na kulazimishwa kufanya kazi.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani, UNICEF iliyotolewa hii Jumanne.
Ripoti hiyo iliyopewa anwani ya "Safari ya Hatari ya Watoto Kupitia Njia ya Wahamiaji ya Mediteranea", inaeleza kwa kina hatari wanazokumbana nazo watoto Waafrika wakimbizi wanaposafiri kupitia jangwa la Sahara hadi Libya na hatimaye kuvuka bahari kuingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediteranea.
Robo tatu ya watoto waliohojiwa wamesema huwa wanakumbwa na manyanyaso na ukatili mikononi mwa watu wazima. Afshan Khan, Mkurugenzi wa UNICEF anayesimamia suala la janga la wahamiaji Ulaya anasema amejionea hali halisi ya watoto hao Italia na ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya utenge fedha kuimarisha mipango ya ulinzi wa mtoto nchini Libya ili kuzuia watoto walio hatarini zaidi na pia kuinua uwezo kwenye vituo vya mapokezi na malezi.
Mapendekezo mengine matano ni ulinzi wa watoto wakimbizi na wahamiaji wanaosafiri peke yao, kutowekwa korokoroni watoto wanaotafuta hifadhi, kuweka familia pamoja kama njia ya kulinda watoto na kuchukua hatua dhidi ya vichochezi vya ukimbizi na uhamiaji.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, katika mwaka huu wa 2017, wahajiri karibu 230 wameaga dunia wakiwa njiani kuelekea katika nchi za Ulaya.
Mashirika ya misaada yanakadiria kuwa watu zaidi ya 5,000 walifariki dunia mwaka uliomalizika wa 2016 katika jitihada za kuingia barani Ulaya.