Mar 02, 2017 02:39 UTC
  • Tunisia na kuendelea matatizo ya kiuchumi

Umoja wa Mataifa umeitahadharisha Tunisia kuhusu kutekeleza siasa za kubana matumizi kufuatia kuendelea matatizo ya kiuchumi nchini humo.

Juan Pablo Bohoslavsky mtaalamu wa kujitegemea kuhusu athari za madeni ya nje na masuala mengine yanayohusiana na masharti ya kifedha kimataifa amesema baada ya kukamilisha kazi ya kutathmini uchumi wa Tunisia kuwa, serikali ya nchi hiyo inapaswa kukabiliana na ongezeko linalotia wasiwasi la nakisi ya bajeti yake kwa msaada wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF); na si kukariri makosa ya zama za utawala wa Zainul Abidin bin Ali Rais wa zamani wa nchi hiyo - aliyeikimbia nchi - kwa kutekeleza siasa za kubana matumizi. Mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi ameongeza kuwa kutekelezwa siasa hizo za kubana matumizi kulizusha malalamiko na upinzani wa wananchi katika miaka kadhaa iliyopita huko Tunisia. Bohoslavsky ametahadharisha kuwa  mafanikio ya demokrasia yaliyopatikana huko Tunisia yatasambaratika iwapo kutajitokeza  mgogoro wa kiuchumi na kijamii huko Tunisia.

Tunisia ni nchi ya kwanza iliyoshuhudia wimbi la maandamano ya mapinduzi ya wananchi baada ya kijana mmoja mchuuzi wa barabarani kuamua kujichoma moto baada ya kuchoshwa na kukosekana usawa wa kiuchumi na uadilifu wa kijamii nchini humo. Hata hivyo nchi hiyo iliweza kwa haraka kutuliza hali ya kisiasa kwa kiwango fulani kwa kuendesha uchaguzi  na kuandaa katiba ili kuboresha hali ya mambo nchini humo. Pamoja na hayo yote, matatizo ya kiuchumi yangali ni changamoto kubwa kwa nchi hiyo. Umaskini, ukosefu wa ajira, ukosefu wa amani na kushindwa kuvutia uwezekaji vitega uchumi kwa ajili ya kujenga miundombinu na kuandaa suhula  muhimu za msingi, yote hayo yamesalia kuwa changamoto kuu kwa Tunisia katika sekta ya uchumi. Hata hivyo sehemu kubwa ya changamoto hizo zinarejea kwa migogoro ya kisiasa na kiusalama inayoitatiza nchi hiyo. Suala la ugaidi ni tatizo kuu linaloikabili nchi hiyo. Katika miaka kadhaa iliyopita, sehemu kubwa ya raia wa Tunisia hususan vijana wamepotoshwa na kujiunga na makundi ya kigaidi kwa kupewa ahadi za kupatiwa fedha na ajira. Katika upande mwingine, Hali ya Tunisia ya kuchangia mpaka wa pamoja  kati yake na Libya na wakati huo huo kuwepo hali ya mgogoro nchini humo, si tu kuwa kumerahisisha harakati za makundi ya kigaidi katika ardhi ya nchi hiyo, bali sehemu ya makundi hayo ya kigaidi yameweka ngome zake katika mipaka ya nchi hiyo. Kukaririwa mashambulizi ya kigaidi miaka kadhaa iliyopita huko Tunisia kunaashiria wazi hatari kubwa ya kujipenyeza magaidi nchini humo. Watu karibu 23 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika jumba la makumbusho ya taifa la Bardo katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis, mwaka 2015. Aidha kushambuliwa hoteli moja katika mkoa wa pwani wa Suisse mashariki mwa nchi hiyo, ni shambulizi jingine la kigaidi lilosababisha vifo an kujeruhi watu wengi wakiwemo raia wa kawaida wa Tunisia na watalii wa nchi za kigeni.

Shambulio la kigaidi katika Jumba la Makumbusho ya Taifa la Bardo, Tunisia 

Matukio hayo yote yalijiri huku ikizangatiwa kuwa sekta ya utalii ndiyo sehemu kubwa zaidi inayodhamini pato la nchi hiyo. Kuendelea ukosefu huo kumepelekea kupungua kiwango cha watalii huko Tunisia na kupungua mapato ya serikali. Muda umepita hadi sasa ambapo hali ya hatari imetangazwa huko Tunisia ili kukabliana na ukosefu wa amani nchini humo; huku hali hiyo ikiwa imeshaoongezwa muda mara kadhaa hadi sasa. Hata hivyo vitisho vya ugaidi vinaendelea kuwa tishio kuu kwa utulivu na amani nchini humo na wakati huo huo vikihesabiwa kuwa moja ya vizuizi vikuu vinavyozuia uwekezaji huko Tunisia. Ni wazi kuwa hali ya uchumi wa Tunisia itaweza kuimarika pale utulivu wa kisiasa utakaporejea na kushuhudiwa amani ya kudumu nchini humo. 

Tags