Dikteta wa zamani wa Tunisia aendelea kuandamwa na vifungo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25926-dikteta_wa_zamani_wa_tunisia_aendelea_kuandamwa_na_vifungo
Dikteta aliyeondolewa madarakani wa Tunisia amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela kutokana na tuhuma za faili jingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 04, 2017 12:32 UTC
  • Dikteta wa zamani wa Tunisia aendelea kuandamwa na vifungo

Dikteta aliyeondolewa madarakani wa Tunisia amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela kutokana na tuhuma za faili jingine.

Mahakama ya Tunisia imemuhukumu kifungo cha miaka sita jela bila ya kuwepo mahakamani dikteta Zine El Abidine Ben Ali, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyeondolewa madarakani na wananchi kwa kupatikana na hatia nyingine ya ufisadi wa fedha za umma. 

Msemaji wa Mwanasheria Mkuu nchini Tunisia, Sufyan al-Saliti amesema kuwa, mahakama ya mwanzo nchini humo imewahukumu watuhumiwa nane akiwemo dikteta huyo katika faili hilo.

Picha ya kumbukumbu ya watawala walioondolewa na wananchi

Imed Trabelsi, mkwe wa Zine El Abidine Ben Ali ni kati ya waliopatikana na hatia ya kuhusika na faili la ufisadi la 'Sherehe za Mariah Carey' mwimbaji maarufu wa nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Sufyan al-Saliti mahakama hiyo imewahukumu watuhumiwa wote vifungo vya miaka sita, huku Trabelsi akihukumiwa kifungo cha miaka 11 jela.

Rais huyo wa zamani wa Tunisia aliyeondolewa madarakani na wananchi na kisha kutoroka nchi, tayari amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kuhusika na mauaji dhidi ya waandamanaji katika harakati za mapinduzi ya mwaka 2011 ambayo yalipelekea zaidi ya watu 300 kuuawa.

Imed Trabelsi, mkwe wa Zine El Abidine Ben Ali

Yapata wiki mbili zilizopita, Zine El Abidine Ben Ali alihukumiwa pia kifungo cha miaka 10 mingine jela kutokana na faili la ufisadi wa mali ya umma. Itakumbukwa kuwa, Ben Ali alilazimika kukimbia nchi hiyo yeye na familia yake hapo tarehe 14 Januari 2011 na kuelekea Saudi Arabia, kufuatia machafuko na maandamano ya wananchi yaliyoenea nchi nzima dhidi ya utawala wake.