Nigeria yawataka raia wake kutosafiri nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26054-nigeria_yawataka_raia_wake_kutosafiri_nchini_marekani
Serikali ya Nigeria imewataka raia wake kujiepusha kusafiri Marekani katika kipindi hiki hadi pale Washington itakapoweka wazi na kutoa ufafanuzi kuhusu sera zake za kigeni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2017 03:51 UTC
  • Nigeria yawataka raia wake kutosafiri nchini Marekani

Serikali ya Nigeria imewataka raia wake kujiepusha kusafiri Marekani katika kipindi hiki hadi pale Washington itakapoweka wazi na kutoa ufafanuzi kuhusu sera zake za kigeni.

Abike Dabiri-Erewa, Msaidizi Maalumu wa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika katika Masuala ya Kigeni amesema kuwa, katika wiki za hivi karibuni, raia wa Nigeria waliokuwa na viza na vyeti vingine halali vya kusafiria wamezuiwa kuingia nchini Marekani na aghalabu yao wamerejeshwa nchini mara tu baada ya kutua katika uwanja wa ndege.

Katika hali ambayo Rais Donald Trump wa Marekani jana alisaini agizo jipya la kuwapiga marufuku raia wa nchi sita za Kiislamu kutosafiri Marekani, Dabiri-Erewa amewataka Wanigeria kutosafiri Marekani katika muda huu isipokuwa tu wenye safari za dharura na za lazima. 

Maandamano dhidi ya Trump na ubaguzi wake nchini Marekani

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015 za Kituo cha Utafiti cha Pew cha Marekani, kati ya wahamiaji milioni 2.1 wa nchi za Afrika wanaoishi Marekani, 327,000 ni raia wa Nigeria. 

Wananchi wa Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen wamepigwa marufuku kuingia nchini Marekani kwenye agizo hilo jipya la Trump huku Iraq ikiondolewa kwenye orodha ya kwanza ya nchi saba zeye idadi kubwa ya Waislamu. 

Ifahamike kuwa, agizo la kwanza dhidi ya wahamiaji na raia wa nchi saba za Kiislamu la Trump liligonga mwamba kutokana na kusimamishwa na mahakama. Kadhalika agizo hilo lilikabiliwa na ukosoaji na maandamano.