Baraza la Usalama la UN lasisitiza mapambano dhidi ya Boko Haram
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa njia ya kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram ni kustawisha eneo la Ziwa Chad.
Taarifa ya ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliolitembelea eneo la Ziwa Chad imesema kuwa: Kunapaswa kuchukuliwa hatua madhubuti za kiuchumi na kijamii ili kuweza kuliangamiza kikamilifu kundi la Boko Haram ambalo limesababisha mgogoro mkubwa wa kiusalama na kibinadamu katika eneo la Ziwa Chad.
Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa pia umelitaka jeshi la mataifa kadhaa yanayopambana na kundi la kigaidi la Boko Haram kudumisha juhudi za kusafisha eneo la Ziwa Chad na kuliangamiza kundi hilo la kigaidi.
Vilevile Baraza la Usalama limetangaza tena uungaji mkono wake kwa nchi wanachama wa Kamisheni ya Ziwa Chad ambazo ni Cameroon, Nigeria, Niger, Chad zinazokabiliana na kundi hilo.
Itakumbukwa kuwa wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walikuwa katika safari ya kuzitembelea nchi nne za eneo la Ziwa Chad. Safari hiyo imefanyika huku eneo hilo likisumbuliwa na changamoto kubwa ya ugaidi na tatizo la wimbi kubwa la wakimbizi.
Lengo la safari hiyo limetajwa kuwa ni kuchunguza mgogoro wa eneo la Ziwa Chad na kuelekeza macho ya walimwengu katika matatizo ya eneo hilo.