Iran na Ivory Coast kuimarisha uhusiano wao wa pande mbili
Mansour Shakib-Mehr, Balozi wa Iran nchini Ivory Coast amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi katika nyuga za uchumi, diplomasia na siasa.
Shakib-Mehr, Balozi wa Iran mjini Abidjan aliyasema hayo jana Ijumaa katika mkutano wake na Marcel Amon-Tanoh, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ivory Coast na kuongeza kuwa, fursa na mazingira yanaruhusu kupanuliwa uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Abidjan katika nyuga mbali mbali, hususan ushirikiano wa kiuchumi, sekta za biashara, nishati, mafuta, gesi, kilimo, uchukuzi, afya na matibabu.
Mansour Shakib-Mehr, Balozi wa Iran nchini Ivory Coast ameeleza juu ya utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu wa kuipa Kodivaa uzoefu wake katika nyuga hizo.
Kwa upande wake, Marcel Amon-Tanoh, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ivory Coast amesema kuwa, uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Abidjan upo katika hatua nzuri na kubainisha kuwa, katika miezi michache ijayo, kamisheni za pamoja za Kodivaa na Iran zitafanya vikao vya kujadili namna ya kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili.
Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Ivory Coast amebainisha kuwa karibuni hivi ataitembelea Iran huku akitumai kuwa maandalizi ya mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif kuitembelea nchi hiyo ya Kiafrika yako katika hatua za mwisho.