Washukiwa 6 wa al Shabab watiwa nguvuni Malindi, Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26248-washukiwa_6_wa_al_shabab_watiwa_nguvuni_malindi_kenya
Polisi ya kupambana na ugaidi ya Kenya imewatia nguvuni watu 6 wanaoshukiwa kuwa magaidi wa kundi la al Shabab katika mji wa pwani wa Malindi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2017 13:19 UTC
  • Washukiwa 6 wa al Shabab watiwa nguvuni Malindi, Kenya

Polisi ya kupambana na ugaidi ya Kenya imewatia nguvuni watu 6 wanaoshukiwa kuwa magaidi wa kundi la al Shabab katika mji wa pwani wa Malindi.

Taarifa zinasema kuwa, polisi wa kikosi hicho maalumu walivamia nyumba mbili usiku wa kuamkia leo katika maeneo ya Shella na Majengo mjini Malindi na kuwatia nguvuni watu 6 wanaoshukiwa kulifadhili kwa fedha kundi la kigaidi la al Shabab. 

Askari polisi hao pia wamekamata simu 7 za kiganjani. 

Inspekta Mkuu wa Jeshi la Polisi la Kenya, Joseph Boinnet ameviambia vyombo vya habari kwamba, watu hao wote wametiwa nguvuni kwa kushukiwa kutuma fedha kwa wanachama wa kundi la kigaidi la al Shabab huko Somalia. 

al Shabab nchini Somalia

Polisi ya Kenya inasema washukiwa hao ni sehemu ya mtandao unaosajili vijana kwa ajili ya kujiunga na kundi la kigaidi la al Shabab. 

Washukuwa hao ambao wanajumuisha wanawake kadhaa wanaaminika kuwa wamekuwa wakilenga wasichana wanaopelekwa Somalia na kuwa wake wa wapiganaji wa kundi la al Shabab.