Afisa wa polisi Tunisia auawa na magaidi
Magaidi wakufurishaji nchini Tunisia wamempiga risasi na kumuua afisa wa polisi nchini Tunisia na kuwajeruhi wengine watatu.
Taarifa zinasema kuwa, magaidi wawili pia waliuawa katika hujuma hiyo iliyojiri katika mji wa Kebili kusini magharibi mwa eneo la jangwani nchini Tunisia.
Magaidi waliwafyatulia risasi maafisa wa polisi wa kulinda doria ambao walikuwa wameweka kambi ya upekuzi katika makutano ya barabara mjini humo.
Tunisia imekuwa ikikabiliana na tishio kubwa la magaidi wakufurishaji ambao mwaka 2015 na mapema mwaka 2016 walitekeleza hujuma dhidi ya watalii katika jengo la makumbusho mjini Tunis na eneo la kitalii mjini Sousse.

Ripoti zinaonesha kuwa, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, raia takribani 6,000 hadi 10,000 wa Tunisia walijiunga katika safu ya makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi za Syria, Iraq na Libya.
Baadhi ya wanachama wa makundi hayo ya kigaidi wameuawa nje ya Tunisia huku 2,000 kati yao wakiwa katika orodha ya waliotoweka bila kujulikana hatima yao. Jambo hilo limepelekea wakuu wa usalama kuingiwa na wasi wasi kuhusu wimbi jipya la hujuma za kigaidi nchini humo.