Katibu Mkuu wa OIC aonana na Rais wa Kodivaa
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC ameonana na Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast na pande mbili zimejadiliana masuala ya kieneo na njia za kupambana na misimamo ya kuchupa mipaka.
Yusuf bin Ahmad al Uthaimin amesema baada ya mazungumzo yake hayo na Rais Alassane Ouattara wa Kodivaa kwamba pande zote mbili zina hamu ya kushirikiana katika nyuga tofauti za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu ina wanachama 57 kutoka mabara manne ya dunia.
Miongoni mwa vipengee vya hati ya jumuiya hiyo ni kuchungwa na kulindwa thamani za kijamii na kiuchumi za ulimwengu wa Kiislamu.
Vipengee vingine vya hati hiyo ni pamoja na kuimarishwa mshikamano baina ya nchi wanachama, kuongezwa kiwango cha ushirikiano katika masuala ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu na kisiasa sambamba na kusaidiana nchi wanachama katika kuleta amani na usalama kimataifa.
Kipengee kingine muhimu cha hati ya OIC ni kunyanyua kiwango cha elimu cha nchi wanachama hususan katika masuala ya sayansi na teknolojia.
Nchi za Uganda na Msumbiji ni miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC zinazofaidika na misaada ya kiuchumi na kielimu ya jumuiya hiyo.