Shambulio la kigaidi laua watu kadhaa Mogadishu, Somalia
Polisi ya Somalia imetangaza kuwa shambulio la kigaidi lililotokea jana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu limeua watu kadhaa na kujeruhi wengine wengi.
Afisa wa polisi ya Mogadishu, Mohamed Adan amesema kuwa shambulio hilo lililofanyika kwa kulipua gari lililokuwa limetegwa mabomu limesababisha vifo vya watu wasiopungua watano na kujeruhi wengine kadhaa.
Amesema mlipuko huo umetokea karibu na ukumbi wa taifa wa michezo ya kuigiza na ikulu ya rais wa nchi hiyo.
Kundi la kigaidi la al Shabab limelaumiwa kuwa ndilo lililofanya hujuma hiyo.
Shambulizi hilo limefanyika masaa machache baada ya Waziri Mkuu Mpya wa Somalia kutangaza baraza lake la mawaziri 26 na kumteua waziri wa zamani wa mambo ya nje kuwa Waziri wa Fedha. Vilevile amemteuwa mwandishi wa habari kuwa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa nchi hiyo.